1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Erdogan atangaza kuwasemehe waliomtusi

30 Julai 2016

Rais wa Uturuki amesema ataondoa mashtaka yote dhidi ya raia waliotuhumiwa kumkashifu, kama ishara ya kipekee. Erdogan pia amewaambia wakosoaji wa kigeni wa safishasafisha inayofanywa na Ankara "kujali ya kwao."

https://p.dw.com/p/1JYmx
Türkei Erdogan
Picha: picture-alliance/AA/A. Izgi

Akizungumza mjini Ankara siku ya Ijumaa, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema uamuzi wake wa kuondoa mashitaka umetiwa motisha na hisia za umoja dhidi ya mapinduzi yaliofeli.

"Kwa mara moja tu, nitakuwa mwenye kusamehe na kuondoa mashtaka yote dhidi ya matukio mengi ya kunikosea heshima na matusi yalioelekezwa kwangu," alisema Erdogan katika tukio la kuwakumbuka wahanga wa jaribio lililofeli la mapinduzi ya kijeshi dhidi yake wiki mbili zilizopita.

Erdogan aliieleza hatua hiyo kuwa ni "mwanzo mpya." "Nahisi kwamba ikiwa hatutatumia fursa hii vizuri, basi tutawapa watu haki ya kutukalia kooni," aliongeza. "Hivyo nahisi kwamba makundi yote ya kijamii, wanasiasa kwanza kabisaa, watajiheshimu kulingana na uhalisia huu mpya, hali hii nyeti iliyo mbele yetu."

Mwandishi wa tashtiti na mtangazaji Jan Böhmermann anakabiliwa na kesi ya kumtukana rais Erdogan.
Mwandishi wa tashtiti na mtangazaji Jan Böhmermann anakabiliwa na kesi ya kumtukana rais Erdogan.Picha: picture-alliance/Eventpress Hoensch

Böhmermann kutoka kitanzini?

Chini ya sheria ya Uturuki, watu wanaokutwa na hatia ya kumtukana rais wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka minne gerezani. Zaidi ya watu 2,000 wameshtakiwa kwa makosa hayo, baadhi yao kuhusiana na maudhui wanazosema walizichapisha kwenye mitandao ya kijamii. Viongozi wa vyama vya upinzani pia ni miongoni mwa washitakiwa.

Katika kesi maarufu zaidi hata hivyo, Erdogan pia alimshtaki mwandishi wa tashtiti na mtangazaji wa Kijerumani Jan Böhmermann kuhusiana na shairi la matusi alilolisoma hewani mwezi Machi, akidokeza kimafumbo kwamba Erdogan anajiamiana na wanyama na kuangalia picha za ngono za watoto. Haikubainika mara moja iwapo tangazo la Erdogan linahusu pia mashtaka ya matusi dhidi ya raia wa kigeni.

Rais Erdogan ameshinda nyingi kati ya kesi hizo, ikiwemo moja dhidi ya mlimbwende wa zamani wa Uturuki kwa kuchapisha shairi kwenye mtandao wa Instagram kuhusu kashfa ya rushwa ya ngazi ya juu. Daktari wa Uturuki alifutwa kazi na kukamatwa baada ya kushirikisha picha zinazomliganisha Erdogan na muiguzaji wa filamu ya "Lord of the Rings" Gollum.

Mwandishi Cengiz Candar ameshtakiwa pia, akituhumiwa kwa kumkashifu Erdogan katika mfululizo wa makala zinazokosoa mgogoro uliyoibuka upya na waasi wa Kikurdi. Mapema mwaka huu, Ankara iliibua tukio la kidiplomasia kwa kumhoji mwandishi wa Kiholanzi mwenye asili ya Uturuki kuhusiana na "tweet" za matusi. Alizuwiwa kwa muda kuondoka nchini Uturuki.

Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim akiongozana na maafisa wa jeshi kabla ya mkutano wa baraza la kijeshi uliolifanyia mabadiliko jeshi hilo.
Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim akiongozana na maafisa wa jeshi kabla ya mkutano wa baraza la kijeshi uliolifanyia mabadiliko jeshi hilo.Picha: picture-alliance/dpa/EPA/Str

Mgawanyiko unaozidi na nchi za Magharibi

Katika hotuba yake aliyoitoa katika ikulu ya rais, Erdogan pia aliwakosoa maafisa wa mataifa ya Magharibi kwa kutoitembelea Uturuki baada ya jaribio la mapinduzi. "Hakuna hata mtu mmoja amekuja kutoa pole ama kutoka Umoja wa Ulaya...au kutoka magharibi," alisema.

Rais pia alizungumzia kelele zinazozidi kupigwa kutokana na timuwatimuwa katika idara za jeshi, mahakama, elimu na vyombo vya habari vya Uturuki. "Baadhi ya watu wanatupa ushauri. Wanasema wana wasiwasi. Jaalini ya kwenu! Angalieni matendo yenu," alisema.

"Hayo mataifa au viongozi wasio na wasiwasi kuhusu demokrasia ya Uturuki, maisha ya watu wetu, mustakabali wake - huku wakijawa na wasiwasi kuhusu hatma ya waliokula njama ya mapinduzi - hawawezi kuwa marafiki zetu."

Erdogan aliapa kuchukuwa hatua zote ndani ya mipaka ya kisheria wakati Uturuki ikatafuta adhabu ya kisheria inayostahili kwa waaandaji wa mapiduzi hayo. Afisa wa Uturuki amesema 3,500 kati ya waliokamatwa wameachiwa sasa baada ya kuhojiwa.

Fethullah Gulen, mhubiri tajiri anaedaiwa kupanga njama ya mapinduzi yaliofeli Uturuki.
Fethullah Gulen, mhubiri tajiri anaedaiwa kupanga njama ya mapinduzi yaliofeli Uturuki.Picha: picture-alliance/dpa/Fgulen.Com

Wafuasi wote wa Gulen wafutwa

Akizungumza katika tukio hilo la kuwakumbuka "Mashujaa wa Julai 15," waziri mkuu Binali Yildirim alisema Uturuki imefanikiwa kuwaondoa maafisa wote walio na mafungamano na Fethullah Gulen kutoka jeshini, baada ya kuwafuta kazi karibu nusu ya majenerali wake kufuatia mapinduzi yaliofeli.

"Tumewasafisha kutoka jeshini,wafuasi wa FETO waliokuwa wanajifanya wanajeshi," alisema Yildirim. Uturuki inamtuhumu Gulen kwa kwendesha kundi la ugaidi la Fethullah (Fethullah Terror Organisation - FETO), madai ambayo anayakanusha.

"Tutayafanya majeshi yetu kuwa imara zaidi na tutafanya kazi kuimarisha usalama wa nchi hii." Uturuki ilitekeleza mabadiliko ya jeshi siku ya Alhamisi baada ya karibu nusu ya majenerali wake 358 kufutwa kazi kwa kushiriki katika jaribio hilo la mapinduzi.

Wote wawili Yildirim na Erdogan walionekana kwenye luninga wakilia wakati wa shughuli hiyo, wakati wahanga wa Julai 15 wakikumbukwa.

Marekani yazidi kukanusha kushiriki njama hiyo

Mapema Erdogan alimshambulia Jenerali wa juu wa jeshi la Marekani alieelezea wasiwasi kuhusu uhusiano wa kijeshi baada ya mapinduzi hayo.

Akinukuliwa na vyombo vya habari vya Marekani, kiongozi wa kamandi kuu ya jeshi la Marekani katika kanda ya Mashriki ya Kati Jenerali Joseph Votel, alisema siku ya Alhamisi kwamba jaribio la mapinduzi na kamatakamata iliyofuatia ya majenerali huenda ikaathiri ushirikiano wa Marekani na Uturuki.

Jenerali wa Marekani Joseph Votel amekanusha kuhusika katika njama ya mapinduzi Uturuki.
Jenerali wa Marekani Joseph Votel amekanusha kuhusika katika njama ya mapinduzi Uturuki.Picha: picture alliance/ZUMA Press/Y. Bogu

"Unaegemea upande wa waliokula njama ya mapinduzi badala ya kulishukuru taifa hili kwa kuishinda njama hiyo," alisema Erdogan katika kituo cha kijeshi mjini Golbasi nje ya Ankara, ambako mashambulio ya angani yaliuwa dazeni kadhaa wakati wa mapinduzi.

Katika hatua iliyoashiria uhusiano unaozidi kuwa wa mashaka kati ya washirika hao wa jumuiya ya kujihami NATO, Jenerali Votel alisema Ijumaa katika taarifa kwamba hakuwa na mkono katika jaribio hilo la mapinduzi.

Utawala wa rais Barack Obama uliingilia kati pia, ambapo msemaji wa ikulu ya White House Eric Shultz alisema tuhuma za rais Erdogan "hazina ukweli hata kidogo." "Obama anamchukulia Erdogan kuwa "mshirika wa karibu," aliongeza msemaji huyo.

Ikulu ya White House ilisema siku ya Ijumaa kuwa maafisa wamepokea nyaraka kutoka serikali ya Uturuki, zikiwa na maombi ya kurejeshwa kwa Gulen kutoka Pennsylvania. "Hilo linashughulikiwa kupitia njia sahihi," alisema Shultz, lakini alikataa kusema ni lini uamuzi wa Marekani utafanywa.

Uturuki ni mwanachama muhimu wa muungano unaoongozwa na Marekani kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Syria, ambapo uwanja wake wa kijeshi wa Incirlik unatumiwa kama kituo cha kuanzishia mashmabulizi dhidi ya kundi hilo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe,DW

Mhariri: Caro Robi