1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Gauck wa Ujerumani ziarani China

21 Machi 2016

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani yuko katika ziara ya siku tano nchini China ambapo Jumatatu amekitembelea chuo cha Chama cha Kikomunisti mjini Beijing katika siku ya kwanza ya ziara yake hiyo nchini humo.

https://p.dw.com/p/1IGxX
Joachim Gauck wa Ujerumani akikaguwa gwaride la heeshima mara baada ya kuwasili Beijing. (20.03.2016)
Joachim Gauck wa Ujerumani akikaguwa gwaride la heeshima mara baada ya kuwasili Beijing. (20.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Gauck amepangiwa kukutana na mkuu wa propanda wa kamati kuu ya chama hicho Liu Yunshan katika chuo hicho kabla ya kukutana na Waziri Mkuu wa China Li Keqian.

Ziada ya masuala mengine yenye maslahi kwa nchi hizo mbili Li na Gauck wanatazamiwa kuzinduwa mpango wa chuo hicho wa kubadilishana wanafunzi kati ya nchi hizo mbili kwa mwaka 2016.Mpango huu wa kubadilishana elimu utahusisha wanafunzi katika ngazi ya shule na vyuo vikuu.

Wakati wa ziara hiyo Gauck yumkini akalizusha suala la wanasheria wanaotetea haki za kiraia wanaokandamizwa na wanaoshikiliwa, suala la uhuru wa kujieleza nchini China na suala la haki za binaadamu kuhusu Wakristo nchini humo.

Duru katika ofisi ya rais huyo zinasema mbali na suala la haki za kiraia katika mazungumzo yake na Rais Xi Jinping na Waziri Mkuu Li Keqiang masuala mengine yanayotarajiwa kuzungumziwa ni mazingira na sera ya kigeni.

Uwazi Faraghani

Wakati wa ziara hiyo Gauck na mwandani wake Daniela Schadt watatembelea jeshi la kuvutia la Terracota katika mji wa Xi'an halikadhalika Mji Uliopigwa Marufuku mjini Beijing. Rais huyo wa Ujerumani anatarajiwa kuitumia ziara hiyo kuimarisha uhusiano wa kisiasa na nchi hiyo ambayo kwa mambo yote mawili kisiasa na kiuchumi ni mshirika muhimu kwa Ujerumani.

Wapiganaji wa jeshi la Terrakotta wa mji wa Xiang wanavyoonekana katika makumbusho China.
Wapiganaji wa jeshi la Terrakotta wa mji wa Xiang wanavyoonekana katika makumbusho China.Picha: picture alliance/dpa/W. Yao

Mchungaji huyo wa Kilutheri wa zamani na mwanaharakati wa haki za kiraia kutoka Ujerumani ya Mashariki ambayo hapo zamani ilikuwa ikijulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani pia atakutana na wasanii na watunzi wa vitabu nchini China.Gauck pia atahudhuria ibada ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Francis wa Asisi katika mji wa Xi'an ambapo anategemewa kuzunngumzia suala la kukandamizwa na kufungwa kwa Wakristo kunakofanywa na serikali ya China.

Watalamu wa masuala ya China wanasema Gauck ataikabidhi serikali ya China orodha ya majina ya wapinzani,wanaharakati wa haki za binaadamu,waandishi wa habari na wanasheria ambao wanaendelea kuteseka chini ya ukandamizaji wa serikali au wakiwa vifungoni.

Hata hivyo tukio hilo halitarajiwi kutangazwa hadharani na badala yake likashughulikiwa chini ya kauli mbiu : "Uwazi Faraghani."

Maandalizi ya ziara hayakuwa rahisi

Maandalizi ya ziara yake hiyo hayakuwa rahisi kwani baadhi ya mada zilioko kwenye agenda zilikuwa tata na nyeti mno kwa upande wa China.

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani (kushoto) na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang mjini Beijing. (21.03.2016)
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani (kushoto) na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang mjini Beijing. (21.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/Wu Hong/Pool

Hata hivyo inaonekana marais wa nchi hizo mbili wanaelewana vizuri katika ngazi ya kibinafsi licha ya ukweli kwamba Raisa Gauck alitumia maneno makali wakati wa ziara ya Xi nchini Ujerumani hapo mwezi wa Machi mwaka 2014.Wakati huo rais huyo wa Ujerumani aliitaka serikali ya China kuongeza juhudi za kuimarisha utawala wa sheria katika nchi hiyo ya Asia Mashariki na kuwakumbusha Wachina kwamba haki za binaadamu hazigawiki.

Katika ngazi ya kibinafsi suala muhimu katika agenda yake linatajwa kuwa ni hotuba anayopanga kuitowa mbele ya wanafunzi 1,000 katika Chuo Kikuu cha Tongji mjini Shanghai hapo Machi 23.Kikiasisiwa na serikali ya Ujerumani hapo mwaka 1907 kama sehemu ya mradi wa kitamaduni chuo hicho leo hii kimesimama kama nguzo ya ushirikiano wa kisayansi kati ya Ujerumani na China.

Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl ni profesa wa heshima katika chuo hicho.

Muswada tata

Katika hotuba yake hiyo Gauck yumkini akataja rekodi mbaya China katika uhuru wa vyombo vya habari vya kimataifa na pia akazungumzia muswada tata wa mashirika yasio ya kiserikali.

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani na mpenzi wake Daniela Schadt mjini Beijing. (21.03.2016)
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani na mpenzi wake Daniela Schadt mjini Beijing. (21.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Iwapo muswada huo utapita na kuwa sheria utapunguza kwa kiasi kikubwa sana shughuli za wakfu na mashirika ya kigeni ambayo yatakuwa chini ya udhibiti wa serikali jambo ambalo linaipa mashaka taasisi ya utamaduni ya Ujerumani ya Goethe na taasisi nyengine za wakfu wa kisiasa za Ujerumani zinazoendesha shughuli zake nchini China.

Gauck amekubali kuitembelea China baada ya kukataa mwaliko wa nchi hiyo mara nyingi.Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na rais wa Ujerumani nchini China baada ya miaka mingi ziara ya mwisho iikiwa ni ile iliofanywa na Horst Koehler hapo mwaka 2007.

Mwandishi : Mohamed Dahman/DW/dpa/

Mhariri :Yusuf Saumu