1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Gauck ziarani Ethiopia

18 Machi 2013

Rais wa shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Joachim Gauck, anafanya ziara rasmi ya siku nne nchini Ethiopia ambako amepangiwa pia kuyatembelea makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.

https://p.dw.com/p/17zRV
Rais Joachim Gauck awasili Addis Abeba pamoja na mwandani wake Daniela Schadt,kwa ziara rasmi ya siku nnePicha: picture-alliance/dpa

Ziara hiyo imeanza rasmi jana kwa karamu ya chakula cha usiku pamoja na Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn. Leo asubuhi, Rais Gauck amekutana na kiongozi mwenzake, Girma Woldegiorgis katika kasri la zamani la mfalme Haile Selassie.

Baadae Rais Gauck alitembelea kiunga cha makaburi na kuweka shada la mauwa juu ya kaburi la kiongozi wa kanisa la kiinjili, Gudina Tumsa, aliyeuliwa mwaka 1979 na utawala wa kijeshi uliokuwa ukiongozwa na Mengistu Hailemariam.

Leo jioni Rais Gauck atayatembelea makao makuu ya Umoja wa Afrika ambako kwanza atakuwa na mazungumzo pamoja na mwenyekiti mpya wa umoja huo Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma na baadaye kuuhutubia Umoja huo.

Ujerumani daima imekuwa ikiusaidia Umoja wa Afrika. Tangu mwaka 2006 jumla ya Euro milioni 170 kutoka fuko la Ujerumani la misaada ya maendeleo zimetolewa kugharimia juhudi za amani na miundo mbinu barani Afrika, katika ujenzi wa chuo kikuu cha nchi za Afrika pamoja pia na miradi ya kilimo.

Suala la haki za binaadam litajadiliwa

Joachim Gauck besucht Äthiopiens Premier Hailemariam Desalegn
Rais Joachim Gauck (kushoto) na waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam DesalegnPicha: Getty Images

Baadae leo, Rais Gauck amepangiwa kukutana na wawakilishi wa mashirika ya jamii, ambayo itakuwa fursa nzuri kwake kuzungumzia mada aipendayo ya "uhuru". Licha ya hayo, mashirika kadhaa ya haki za binaadamu tangu ya Ujerumani mpaka na yale ya Ethiopia, yamemkabidhi Rais Gauck risala za malalamiko. Mashariki hayo yanamtaka Rais Gauck apiganie kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa na waandishi habari nchini Ethiopia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani, dpa, Rais Gauck amepanga kulizusha suala la haki za binaadamu atakapozungumza na viongozi wa serikali ya Ethiopia. Hata wawakilishi wa kidini wanapanga kukutana na rais huyo wa Ujerumani.

Ziara hii inafanyika katika wakati ambapo Ujerumani inaadhimisha mwaka mmoja tangu Rais Joachim Gauck akabidhiwe wadhifa huo na mjadala kupamba moto kuhusu madaraka ya rais humu nchini.

Rais Gauck anayefuatana na mwandani wake Daniela Schadt katika ziara yake hii ya kwanza barani Afrika, anatarajiwa kurejea mjini Berlin Jumatano usiku.

Mwandishi: Ludger Schadomsky/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef