1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Karzai asisitiza majeshi yake kushika hatamu ya ulinzi 2014

20 Julai 2010

Majeshi ya NATO yasisitiza kuendelea kubaki Afghanistan

https://p.dw.com/p/OPoM
Rais Hamid Karzai, wa pili kushoto,na Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton,kulia, wakitembelea duka la bidhaa za kazi za mikono,jijini Kabul,Siku ya Jumanne,tarehe 20, Julai,2010,wakiwa bado katika mkutano wa kimataifa unaojadili hali ya baadaye ya Afghanistan.Picha: AP

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai,ameueleza mkutano wa kimataifa wa siku moja unaofanyika jijini Kabul,kuwa majeshi ya nchi yake,yatakuwa tayari yameiva kiasi cha kuweza kushika hatamu ya ulinzi na usalama nchini humo,ifikapo mwaka 2014.

Pamoja na mambo mengine ajenda ya haki za msingi za wanawake wa Afghanistan,nayo imepewa kipaumbele na serikali ya Marekani katika mkutano huo.

Licha ya kauli ya Rais Karzai juu ya msimamo wa serikali yake kuweza kusimamia suala la ulinzi na usalama ifikapo mwaka 2014,lakini Katibu mkuu wa majeshi ya NATO,huko Afghanistan Anders Fogh Rasmussen,amesisitiza kuwa majeshi hayo yataendelea kuwepo Kabul,katika kipindi hicho cha mpito.

Mkutano huo unaohudhuriwa na wawakilishi zaidi ya 70 kutoka jumuiya za kimataifa,wakiwemo mawaziri wa kigeni 40.

Rasmussen ameeleza kuwa majeshi ya kujihami ya nchi za magharibi,NATO yataendelea kusaidia majeshi ya Afghanistan,hata baada ya kukabidhiwa jukumu la kusimamia ulinzi nchini humo,litakaporejeshwa mikononi mwa jeshi la nchi hiyo,na kueleza zoezi la kuondoa litafanyika kwa awamu,ili kuyapa muda majeshi ya nchi hiyo kuweza kushika hatamu ya ulinzi.

Ameeleza kuwa wakati huo utapofika,majeshi ya kimataifa hayataondoka moja kwa moja,akielezea kuwa kuwepo kwa hali ya ilivyo sasa,kumechangiwa na majeshi hayo,hivyo hawawezi kuondoka kwa mkupuo,na kuiacha nchi hiyo bila kuwa na uhakika kamili wa usalama na uwezo wa majeshi yao,kusimamia ulinzi.

Imeelezwa kuwa zaidi ya wanajeshi 140,000 wa Marekani na NATO,yapo Afghanistan,lakini idadi hiyo inatajwa kuwa itaweza kuongezeka na kufikia 150,000 ifikapo mwezi August mwaka huu,katika kipindi cha operesheni maalumu itakayofanywa na majeshi hayo katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.

Rasmussen amesisitiza kwamba majeshi ya NATO hayataruhusu kundi la Taliban,kuiondoa serikali iliyo madarakani kwa kutumia nguvu,na kueleza pia majeshi hayo yatahakikisha kwamba mtandao wa Al Qaeda hauwezi kuitawala tena nchi hiyo kama ilivyokuwa hapo awali.

Amezidi kuwahakikishia wananchi wa Afghanistan kuwa wataendelea kuwa nao bege kwa bega kwa kipindi kirefu zaidi,hata baada ya kumalizika rasmi kwa muda wa majeshi hayo kuwepo Afghanistan.

Akionekana kuwa amedhamiria juu ya azma ya majeshi yakulinda amani nchini humo kuwa bado yataendelea kuwasaka Taliban na kuuvunja kabisa mtandao wa Al Qaeda,Rasmussen ameeleza kuwa msimamo huo,uwafikie wananchi wa Afghanistan,na pia iwe ni salamu kwa maadui wa amani nchini humo.

Wakati huo huo,Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani,Hillary Rodham Clinton amewaambia wanawake wa Afghanistan kuwa nchi yake haitawatenga wanawake,katika vita dhidi ya kundi la uasi la Taliban,kwa kutafuta njia muafaka ya kisiasa.

Clinton,ambaye moja ya ajenda yake kuu kisiasa ni kuwakwamua wanawake kiuchumi na kuwatoa katika makucha ya kunyanyaswa,na kueleza kuwa zama za unyonge wa wanawake wa Afghanistan zinaelekea kumalizika.

Chini ya utawala wa Taliban,wanawake nchini humo hawakuruhusiwa kufanya kazi na kupata elimu,hivyo Clinton amesisitiza kuwa,uzoefu mkubwa alio nao katika kutatua migogoro mbalimbali katika maeneo ya Amerika ya Kusini,Ireland ya kaskazini na Afrika,unaonyesha kuwa siri ya mafanikio ya kiuchumi nchini humo,ni lazima kuwashirikisha wanawake katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Ameahidi kutumia ushawishi huo,kuwakwamua wanawake wa Afghanistan.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa /Reuters/DPA

Mhariri:Abdul-Rahman