1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Lourenco: Hakuna mazungumzo na Dos Santos

Daniel Gakuba
3 Februari 2020

Katika mahojiano maalum na DW, Rais wa Angola Joao Lourenco amezungumzia shutuma za ubadhirifu nchini mwake, na mchango wake kama afisa wa ngazi ya juu chini ya ungozi wa Jose Edourado dos Santos.

https://p.dw.com/p/3XBae
João Lourenço, Präsident von Angola, im Gespräch mit DW
Rais wa Angola, Joao LourencoPicha: DW/M. Luamba

Katika mahojiano maalum na mwandishi wa  DW, Adrian Kriesch, Rais Joao Lourenco amesema hakuna yeyote aliye juu ya sheria Angola. Haya yanafuatia shutuma za ubadhirifu ambazo zimeiandama serikali yake tangu ilipoingia madarakani mwaka 2017, licha ya ahadi zake wakati wa kampeni kwamba angeleta mageuzi ya kiuchumi na kupambana na ufisadi.

Habari iliyogonga vichwa vya habari hivi karibuni ni kashfa ya Isabel dos Santos, binti wa rais wa zamani wa Angola, Jose Edouardo dos Santos ambaye anaelezwa kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika. Isabel anatuhumiwa kutumia ushawishi wa baba yake kujenga himaya ya kiuchumi yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni mbili.

Upotevu wa mamilioni ya Dola

Mnamo wiki chache zilizopita, ripoti ya wachunguzi wa kimataifa ilibainisha kuwepo njama ya kuyachota mamilioni ya dola kutoka hazina ya serikali na kuhamishiwa katika akaunti za watu binafsi kupitia hila zinazowahusisha maafisa wa serikali.

Isabel dos Santos angolanische Investorin
Isabel dos Santos, anatuhumiwa kutumia ushawishi wa baba yake kujitajirishaPicha: picture-alliance/dpa/V. Sharifulin

Aidha, tetesi zilienea kuwa mshukiwa mkuu katika njama hizo, Isabel dos Santos, alikuwa akijadiliana na serikali ili aweze kuzirudisha fedha anazodaiwa kuziiba. Katika mazungumzo na DW, Rais Lourenco amesema taarifa zote hizo hazina msingi.

''Tungependa kusema wazi kuwa hakuna majadiliano, na hakutakuwepo majadiliano. Watu wanaohusika walipewa muda wa miezi sita kurejesha mali waliyoipata kwa njia haramu kutoka hazina ya taifa. Wale ambao hawakuutumia muda huo, watawajibika kwa hatua zinazoweza kufuata.'' Amesema Lourenco.

Isabel ajikuta matatani

Mali ya Isabel iliyoko nchini Angola hivi sasa inashikiliwa, na tarehe 22 Januari mwendesha mashtaka mkuu alimfungulia mashtaka ya utakatishaji wa fedha, matumizi mabaya, kughushi nyaraka pamoja na uhalifu mwingine wa kifedha alipokuwa kiongozi wa kampuni ya taifa ya mafuta ya Angola.

João Lourenço, Präsident von Angola, im Gespräch mit DW
Rais Lourenco katika mahojiano maalum na Adrian Kriesch wa DW mjini LuandaPicha: DW/M. Luamba

Alipoulizwa kama angependa kumwona Isabel dos Santos akipandishwa kizimbani, Rais Lourenco amesema hiyo ni kazi ya mahakama, sio ya mwanasiasa. Jibu lilikuwa hilo hilo, alipoulizwa ikiwa mtangulizi wake, Jose Edouardo dos Santos anaweza kufunguliwa mashtaka baada ya kinga ya miaka mitano kumalizika.

Amesema, ''Ni taasisi za kisheria ambazo huwachunguza washukiwa wa uhalifu. Kazi ya wanasiasa ni kuweka sera ambazo zinahakikisha uhuru wa mahakama, na kuzifanya mahakama kufanya kazi ndani ya mipaka yake. Rais hawapeleki watu mahakamani. Kuna kesi nyingi nchini.

Na alipoulizwa kuhusu shutuma za upinzani kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika mfumo wa mahakama, Rais Lourenco amesema hiyo sio kweli. Aidha, amekiri mchango wake kama afisa wa ngazi ya juu katika serikali ya mtangulizi wake, na kusema uzoefu huo umemwezesha kujua kuwepo kwa ufisadi katika ngazi za juu, ambao sasa anasema amepata fursa ya kuupiga vita.