1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahama atapambana na mpinzani wake katika uchaguzi wa 2016

23 Novemba 2015

Chama tawala nchini Ghana cha NDC kimempitisha Rais wa sasa wa nchi hiyo, John Mahama kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika mwakani nchini humo.

https://p.dw.com/p/1HAnN
Rais wa sasa wa Ghana, John Mahama.
Rais wa sasa wa Ghana, John Mahama.Picha: DW

Wengi wanatarajia uchaguzi wa mwakani kuwa mgumu kwa bwana Mahama, ambaye utawala wake wa sasa umegubikwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi na tayari amesaini makubaliano na shirika la kimataifa la fedha duniani ili kuweza kusaidia katika bajeti ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka mitatu.

Mahama ambaye amepitishwa na chama chake kwa asilimia 95.1 za kura zilizohesabiwa hapo jana, amesema hatua hiyo , imemuongezea nguvu ya kupambana na changamoto zilizopo na zitakazojitokeza katika kuboresha maisha ya wananchi wa taifa hilo.

"Tumekuwa na changamoto mbalimbali katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ikiwa ni pamoja na migomo kadhaa nchi nzima, hali mbaya ya kiuchumi, na kibaya zaidi matatizo ya umeme ambayo hadi sasa bado yanatukabili" alisema Mahama wakati alipozungumza na wanachama wa chama chake mara baada ya matokeo kutangazwa.

Ghana ni mfano wa kuigwa kidemokrasia barani Afrika

Ghana ni taifa ambalo linachukuliwa kama mfano wa kuigwa katika masuala ya demokrasia barani Afrika kwa sababu ya kufanya uchaguzi katika mazingira ya amani,mabadiliko ya mara kwa mara ya kupokezana madaraka na utii wa sheria.

Hata hivyo tangu mwaka 2013, taifa hilo limekuwa likikabiliana na hali mbaya ya kiuchumi, kukuwa kwa deni la taifa na mfumuko wa bei hali iliyoathiri pia kushuka kwa thamani ya fedha ya nchi hiyo kwa asilimia 30.

Mahama aliahidi kujitahidi kupunguza umasikini, kutengeneza nafasi zaidi za ajira na kuongeza kuwa wananchi wa Ghana wanapaswa kuwa na imani na serikali yake.

Mahama alikuwa ni mgombea pekee wa nafasi hiyo katika chama chake katika uchaguzi uliofanyika katika vituo 8,000 ambapo wagombea 275 wa viti mbalimbali vya ubunge ndani ya chama hicho walichaguliwa pia kuwania nafasi hizo katika uchaguzi huo wa mwakani.

Mpinzani wake katika kinyanganyiro hicho Nana Akufo-Addo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 71 alipata asilimia 96 ya kura kupitia chama chake cha New Patriotic Party katika uchaguzi uliofanyika mwaka mmoja uliopita.

Mwandishi: Isaac Gamba/RTRE
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman