1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Medvedev awaonya wanamgambo

Kabogo Grace Patricia31 Machi 2010

Onyo hilo amelitoa kufuatia mashambulio yaliyotokea siku ya Jumatatu huko Moscow na leo Jumatano huko Dagestan.

https://p.dw.com/p/MjLG
Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev.Picha: AP

Rais Dmitry Medvedev wa Urusi amesema wanamgambo hawataruhusiwa kueneza hofu nchini humo kutokana na mfululizo wa mashambulio ya mabomu yaliyotokea wiki hii nchini Humo. Baada ya mashambulio ya Jumatatu yaliyowauwa watu 39 mjini Moscow na leo mashambulio mengine  huko Dagestan yalipoteza maisha ya watu 12.

Shirika la habari la RIA-Novosti limemnukuu Rais Medvedev akisema kuwa malengo ya magaidi ni kuchochea ghasia nchini Urusi, kuvunja vyama vya kiraia, kueneza hofu na wasi wasi miongoni mwa watu wa nchi hiyo. Akizungumza hii leo, Rais Medvedev amesema serikali yake haitaruhusu vitendo kama hivyo kutokea na kwamba kila kitu watakachofanya kitakuwa na lengo la kujizatiti zaidi. Rais Medvedev amesema mashambulio mawili ya kujitoa mhanga yaliyotokea siku ya Jumatatu mjini Moscow na mashambulio mengine yaliyotokea hii leo huko Dagestan yamefanywa  na watu wa  mtandao mmoja.

Mashambulio ya Dagestan yamesababisha vifo vya watu 12  na kuwajeruhi wengine . Mashambulio ya leo yametokea ikiwa ni siku mbili tu, baada ya mashambulio mengine mabomu kutokea katika mji mkuu wa Urusi, Moscow kwenye eneo la treni za chini ya ardhi na kuwauwa watu 39. Waziri Mkuu wa Urusi, Vladmir Putin pia anayahusisha mashambulio yote hayo, akisema kundi moja ndilo linahusika. Putin alisema wanaamini kuwa mashambulio yote hayo yalikuwa yakiwalenga wananchi wa Urusi. Kauli za Bwana Putin zilinukuliwa na shirika la habari la Urusi-Interfax. Waziri Mkuu huyo wa Urusi amemuamuru Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Rashid Nurgaliyev kuongeza askari polisi katiak mkoa wa Caucasus Kaskazini kufuatia mashambulio ya leo.

Shirika la ujasusi la Urusi-FSB limeyatuhumu makundi ya kigaidi ya Caucasus Kaskazini kuwa yanahusika na mashambulio hayo. Mkuu wa baraza la usalama la Urusi, Nikolai Patrushev, alisema nchi hiyo itafanya kila iwezalo kuhakikisha viongozi wa makundi hayo, hasa Doku Umarov, wanafikishwa katika vyombo vya sheria. Hata hivyo, afisa wa kundi la kutetea haki za binaadamu la Chechnya, Nurdi Nurkhashiyev na Rais wa bunge la Chechnya, Dukuwakha Abdurakhmanov wameonya dhidi ya kutolewa hukumu mapema. Kwa upande wake Umarov amekanusha kuhusika na mashambulio hayo.

Shambulio la kwanza hii leo lilifanywa na mshambuliaji aliyekuwa amevalia sare za polisi huko Kizlyar, Dagestan karibu na ofisi za FSB na Wizara ya mambo ya ndani zilizoko katika eneo hilo. Bomu la mshambuliaji huyo linaripotiwa kuwa na uzito wa kilo 200 na liliwashwa karibu na shule, ingawa hakukuwa na wanafunzi wakati huo. Muda mfupi baadaye mshambuliaji wa pili alijitoa mhanga kwa kujiripua katika eneo jingine la Kizlyar baada ya polisi kulisimamisha gari lake katika kizuizi. Askari polisi wawili na abiria mmoja waliuawa katika mripuko huo. Baada ya umati wa watu kufurika katika eneo la ukio, mshambuliaji mwingine aliyekuwa amevalia sare za polisi alijiripua. Wengi wa waliouawa katika mashambulio hayo mawili walikuwa askari polisi.

Aidha, Rais Medvedev amewaamuru maafisa wa Dagestan kutoa msaada kwa familia za watu waliathirika na mashambulio hayo. Maeneo ya Dagestan na mkoa wa Caucasus Kaskazini mara nyingi yamekuwa kituo cha mapigano kati ya vikosi vya jeshi la Urusi na waasi wa Kiislamu. Mwaka uliopita pekee zaidi ya maafisa wa usalama na waasi 1,000 waliuwawa katika mapigano. Kwa sasa serikali ya Urusi imeweka wanajeshi 23,000 katika mkoa huo katika hatua za kujaribu kulidhibiti eneo hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed