1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Morales ashinda muhula mwingine Bolivia

25 Oktoba 2019

Rais wa Bolivia Evo Morales ameshinda kwa awamu ya nne katika uchaguzi wa rais wa duru ya kwanza ulioandamwa na kiwingu cha madai ya wizi wa kura na ambao matokeo yake yanapingwa na upande wa upinzani.

https://p.dw.com/p/3RuDc
Bolivien Präsidentschaftswahlen Evo Morales Jubel Pose
Rais Evo Morales wa BoliviaPicha: Reuters/D. Mercado

Kulingana na matokeo rasmi yaliyotolewa baada ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa, Morales, mwanasiasa wa mrengo wa shoto amepata asilimia 47.1 ya kura dhidi ya asilimia 36.5 ya mgombea wa siasa za wastani za mrengo wa kulia, Carlos Mesa.

Ushindi huo mwembamba umemwezesha Morales kuongoza kwa asilimia kumi kiwango kinachohitajika kuzuia kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi.

Morales tayari alijitabiria ushindi siku ya Jumatano na kurejea matamshi yake jana Alhamisi saa chache kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo ya uchaguzi.

Wafuasi wa Morales walikusanyika kwenye kitongoji cha Cochabamba kushangilia ushindi wake wakipaza sauti na kusema "Udumu mchakato wa Mabadiliko, Udumu Evo Morales"

Maandamano ya kupinga matokeo yafanyika Bolivia

Bolivia imeshuhudia siku nne za maandamano ya umma dhidi ya madai kuwa serikali ilikuwa inafanya njama za kuiba kura.

Bolivien La Paz Carlos Mesa
Mgombea wa upinzani, Carlos MesaPicha: Getty Images/AFP/J. Bernal

Mgombea wa upinzani ambaye pia ni rais wa zamani wa nchi hiyo, Carlos Mesa,aliituhumu tume ya uchaguzi kufanya udanganyifu wakati iliposhindwa kuendelea kuchapisha matokeo ya uchaguzi yaliyoashiria uwezekano wa kufanyika kwa duru ya pili.

Tume ya uchaguzi ilitumia zaidi ya saa 24 kuhesabu sehemu ndogo ya kura  hatua iliyozusha maandamano ya umma yaliyodai kuna mipango ya kufanyika wizi wa kura ambapo ofisi za tume hiyo na zile za chama cha Morales zilishambuliwa.

Mesa amewataka wafuasi wake kuendelea na maandamano ya amani hadi pale duru ya pili ya uchaguzi itakapokubaliwa.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari mjini La Paz Mesa alisema "Kwanza, ni kushinikiza kuitishwa haraka kwa duru ya pili ya uchaguzi utakaosimamiwa kwa njia sahihi, huru na isiyoegemea upande wowote. Pili ni kuwatolea wito raia, mashirika ya kiraia na watu mashuhuri, kujiunga na mratibu wa ulinzi wa demokrasia na kuendelea kujikusanya kwa amani hadi pale matakwa ya watu walio wengi yatakapoheshimiwa"

OAS na Umoja wa Ulaya wahimiza duru ya pili

Bolivien La Paz Demonstration von Anhängern des Oppositionskandidaten Carlos Mesa und Anhängern von Präsident Morales
Maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguziPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Saenz

Wito wa kufanyika duru ya pili ulitolewa pia na jumuiya ya mataifa ya Bara Amerika ya OAS mnamo siku ya Jumatano.

Umoja wa Ulaya umesema jana unakubaliana na tathmini ya OAS kuwa chaguo sahihi ni kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi ili kurejesha imani ya umma na kuhakikisha uamuzi wa kidemokrasia wa watu wa Bolivia unaheshimiwa.

Kadhalika kanisa katoliki nchini Bolivia na asasi 19 zisizo za kiserikali pia zimetaka kuwepo kwa duru ya pili.

Hata hivyo rais Morales ameutaja msimamo huo wa upinzani kuwa jaribio la kufanya mapinduzi kwa msaada kutoka nje na kuagiza waangalizi wa uchaguzi kutoka jumuiya ya OAS wachunguzwe.