1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Malawi ahimiza maridhiano

8 Aprili 2012

Rais mpya wa Malawi Joyce Banda, ameapishwa kushika madaraka, na kuwaambia wafuasi wake kuwa hakuna nafasi ya kulipiza kisasi, baada ya kifo cha mtangulizi wake Bingu wa Mutharika ambaye alisababisha mgawanyiko.

https://p.dw.com/p/14ZRt
Joyce Banda , rais mpya wa Malawi
Joyce Banda , rais mpya wa MalawiPicha: Reuters

Rai yake kutaka maridhiano inafuatia siku mbili za njama za kisiasa ambazo ziliendeshwa na wafuasi wa Rais aliyefariki, Bingu wa Mutharika, kutaka kumzuia Joyce Banda kuchukua madaraka ya urais, ambayo ni wajibu wake kikatiba kama mtu aliyekuwa makamu wa rais.

Kiapo cha rais huyo ambaye ni wa pili wa kike barani Afrika kililakiwa kwa vifijo na nderemo. Aliwaomba watu kusalia kimya kumkumbuka wa Mutharika aliyemuita baba wa taifa, ingawa hakutafuna ulimi alipozilaumu sera za marehemu mtangulizi wake huyo ambazo ziwagawa watu.

Hayati Bingu wa Mutharika, aliyekuwa rais wa Malawi
Hayati Bingu wa Mutharika, aliyekuwa rais wa MalawiPicha: Reuters

Mustakabali mwema pamoja

''Nataka wote tusonge mbele kuelekea kwenye mustakabali wenye matumaini, tukiwa na moyo wa umoja''. Alisema bi Joyce Banda. Rais huyo ambaye alifukuzwa na wa Mutharika katika chama, alisema ana matumaini kuwa nchi itakuwa na umoja.

Rais Bingu wa Mutharika alifariki Alhamisi kutokana na mshtuko wa moyo. Alikabiliwa na shinikizo kumtaka aachie madaraka, baada ya maandamano makubwa ya mwaka jana, yaliyoandaliwa na watu wanaomshutumu kuharibu uchumi na kuivuruga demokrasia.

Baada ya kufukuzwa na Bingu wa Mutharika kutoka chama Demokrasia na Maendeleo (DPP), bi Joyce Banda aliunda chama chake cha People's Party, hatua ambaye ilichukuliwa na wafuasi wa wa Mutharika kama sababu inayomnyima haki ya kuchukua wadhifa wa urais.

Mkutano kuthibitisha mamlaka

Lakini kufuatia mbinyo kutoka nchi za magharibi na za kiafrika kutaka utulivu wakati wa kupokezana madaraka, Banda ambaye alisindikizwa na wakuu wa jeshi na polisi aliitisha mkutano wa baraza la mawaziri ili kuthibitisha madaraka yake.

Alisema anawashukuru raia wa Malawi na wakazi wa nchi hiyo kwa kuheshimu sheria na kufanikisha mchakato wa kupokezana madaraka katika mazingira yenye utulivu.

Wakati huo huo askari walishika doria kwenye majengo ya bunge na kuimarisha ulinzi wa kituo cha Redio na Televisheni huku jeshi likiunga mkono wazi wazi serikali ya kiraia. Malawi imetangaza siku 10 za maombolezo kwa hayati wa Mutharika, lakini utaratibu wa mazishi yake haujatangazwa bado.

Rais wa 2 mwanamke Afrika

Joyce Banda ni mwanamke wa pili barani Afrika kuwa rais baada ya Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia. Anakabiliwa na changamoto ya kuiongoza nchi ambayo bunge lake linadhibitiwa na chama cha marehemu mtangulizi wake, na upinzani wa wazi katika baraza la mawaziri.

Hayati wa Mutharika alisifiwa kuboresha kilimo
Hayati wa Mutharika alisifiwa kuboresha kilimoPicha: DW

Bingu wa Mutharika ambaye zamani alikuwa mwanauchumi katika Benki ya Dunia, aliingia madarakani mwaka 2004, na kuchaguliwa tena kwa kura nyingi mwaka 2004. Hata hivyo alikosolewa na vyombo vya habari kama mtu ambaye hakupenda kukosolewa.

Baada ya kifo chake, pande mbali mbali zilituma salamu za rambi rambi na kumsifia kwa mafanikio kadhaa, yakiwemo yale ya kuboresha kilimo na kuwenga usalama wa chakula nchini mwake,

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amekaribisha upokezanaji madaraka kwa njia ya amani nchini Malawi, na kuahidi ushirikiano kwa serikali mpya inayoongozwa na kaimu rais, bi Joyce Banda.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Bruce Amani