1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mursi afuta tamko la kujilimbikizia madaraka

9 Desemba 2012

Rais Mohamed Mursi wa Misri amefuta tamko lake ambalo limempa madaraka makubwa na kuzusha ghasia nchini humo lakini amekataa kuchelewesha kura ya maoni juu ya katiba mpya ambalo ni dai kuu la wapinzani wake.

https://p.dw.com/p/16ynI
Ni ukuta wa Ikulu mjii Cairo uliochorwa picha za kuwakejeli Rais Mohamed Mursi, Jemadari Mkuu Mohamed Hussein Tantawi na Rais wa zamani Hosni Mubarak.
Ni ukuta wa Ikulu mjii Cairo uliochorwa picha za kuwakejeli Rais Mohamed Mursi, Jemadari Mkuu Mohamed Hussein Tantawi na Rais wa zamani Hosni Mubarak.Picha: Reuters

Wafuasi wake wa itikadi kali za Kiislamu wamekuwa wakisisitiza kwamba kura hiyo ya maoni ifanyike kama ilivyopangwa hapo tarehe 15 mwezi wa Disemba kwa hoja kwamba inahitajika ili kukamilisha mchakato wa kidemokrasia baada ya kupinduliwa kwa dikteta Hosni Mubarak miezi 22 iliopita.Ahmed Said mwanachama mwandamizi wa upinzani mkuu wa muungano wa Salvation Front amesema uamuzi wa kuendelea na kura hiyo ya maoni ni wa kufadhaisha na utazidi kuuchochea mzozo huo wa kisiasa.Said kiongozi wa kiliberali wa chama cha Free Egyptians ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters "Uamuzi huo unazidi kuyafanya mambo kuwa magumu na siamini kwamba baada ya yote hayo wanataka kupitisha katiba ambayo haiwakilishi Wamisri wote."

Mazungumzo ya kitaifa

Tangazo kwamba Mursi amefuta tamko lake hilo la tarehe 22 mwezi wa Novemba limefuatia mazungumzo ya Jumamosi(08.12.2012) ambayo yaliendelea hadi usiku katika kasri lake la rais. Mazungumzo ya mkutano huo yaliopewa jina kuwa ''mazungumzo ya kitaifa'' yalisusiwa na wapinzani wake wakuu na hayana uzito miongoni mwa waandamanaji katika taifa hilo la Kiarabu lenye idadi kubwa ya watu.Vuguvugu la tarehe 6 mwezi wa April ambalo lilisaidia kuandaa maandamano dhidi ya Mubarak limesema katika taarifa kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo ya Jumamosi kwamba ''kile kilichotokea ni kuendelea kutumia hila kwa jina la sheria na uhalali.''

Rais Mursi akiwa katika mkutano wa mazungumzo ya kitaifa mjini Cairo Jumamosi.
Rais Mursi akiwa katika mkutano wa mazungumzo ya kitaifa mjini Cairo Jumamosi. (08.12.2012)Picha: Reuters

Katiba hiyo ilitayarishwa kwa haraka na jopo lililokuwa likiongozwa na chama cha Udugu wa Kiislamu na Waislamu wengine wa itikadi kali. Waliberali na watu wa misimamo mingine walisusia jopo hilo kwa hoja kwamba sauti zao hazikusikilizwa.Hermes Fawzi muandamanaji mwenye umri wa miaka 28 aliepiga kambi nje ya kasri la rais pamoja na wenzake wengine kadhaa amesema katiba isiokuwa na muafaka haiwezi kupigiwa kura ya maoni na kwamba sio busara sehemu moja tu ya jamii inaachiliwa kutayarisha katiba.

Jeshi latilia mkazo mazungumzo

Vifaru na magari ya kijeshi yamewekwa karibu na kasri hilo ili kulilinda baada ya mapambano wiki iliopita kati ya Waislamu wa itikadi kali na mahasimu zao kuuwa watu saba na kuwajeruhi wengine 350.Jeshi ambalo liliongoza Misri wakati wa kipindi cha mpito baada ya kuanguka kwa Mubarak limeningilia kwenye mzozo hao hapo Jumamosi kwa kuyaambia makundi yanayofarakana kwamba mazungumzo ni muhimu na njia pekee ya kuiepusha nchi hiyo na balaa.

Wanajeshi wa Misri wakilinda Kasri la Rais mjini Cairo.
Wanajeshi wa Misri wakilinda Kasri la Rais mjini Cairo.Picha: AFP/Getty Images

Tamko jipya la Mursi limeondowa baadhi ya vipengele vya tamko la zamani ambavyo vimewakasirisha wapinzani, ikiwa ni pamoja na kipengele ambacho kimempa Mursi madaraka makubwa ya kukabiliana na hatua zinazotishia mapinduzi na usalama wa taifa ambapo wapinzani wanasema kimempa mamlaka ya kufanya atakavyo. Kipengele kengine katika tamko la awali kiliyawekea kinga maamuzi yake dhidi ya pingamizi zozote zile za kisheria hadi hapo litakapochaguliwa bunge jipya jambo ambalo linaonyesha jinsi Mursi asivyoziamini asasi za kisheria kutoka enzi ya Mubarak ambazo kwa kiasi kikubwa hazikufanyiwa mageuzi.Kipengele hicho hakikurudiwa lakini tamko jipya limesema ''matamko ya kikatiba likiwemo tamko hili" haliwezi kutenguliwa na mahakama.Tamko hilo jipya linaelezea hatua za kuunda jopo la kurasimu katiba mpya iwapo rasimu ya sasa itakataliwa.

Taifa limegawika

Wakati wapinzani wa Mursi wakitaka kuanguka kwa utawala wake wafuasi wake Waislamu wa itikadi kali wamesema kuna njama ya kumuangusha rais huyo wa kwanza aliechaguliwa chini ya misingi ya demokrasia nchini humo.Machafuko hayo ya kisiasa yameonyesha mgawanyiko mkubwa katika taifa hilo lenye watu milioni 83 kati ya Waislamu wa itikadi kali ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakikandamizwa na mahasimu zao ambao wana hofu kwamba wahafidhina wa kidini wanataka kuzizima sauti nyengine zote na kuuwekea vikwazo uhuru wa kijamii. Wanachotaka Wamisri wengi ni kuwa tu na utulivu na kufufuliwa kwa uchumi wa nchi hiyo.

Waandamanaji wanaompinga Mursi nje ya kasri lake mjini Cairo.
Waandamanaji wanaompinga Mursi nje ya kasri lake mjini Cairo.Picha: Reuters

Mwandishi: Mohamed Dahman /RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo