1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Musharraf kuvunja bunge la Pakistan

P.Martin6 Novemba 2007

Serikali ya Pakistan imeahidi kulivunja bunge hadi tarehe 15 Novemba na kuitisha uchaguzi mkuu kati kati ya mwezi Januari,licha ya amri ya hali ya hatari iliyotangazwa na Rais Jemadari Pervez Musharraf.

https://p.dw.com/p/C77D
Rais Jemadari Pervez Musharraf akitangaza amri ya hali ya hatari tarehe 3 Novemba mjini Islamabad
Rais Jemadari Pervez Musharraf akitangaza amri ya hali ya hatari tarehe 3 Novemba mjini IslamabadPicha: AP

Akiendelea kulaumiwa na jumuiya ya kimataifa,Rais Musharraf amesema,atajiuzulu kama mkuu wa majeshi na ataongoza kama rais wa kiraia. Kwa upande mwingine,wanasheria na wafanyakazi wa vyombo vya habari wamejeruhiwa katika mapambano na polisi wa kuzuia ghasia.Machafuko hayo yalizuka wakati wa maandamano yaliyofanywa katika miji ya Lahore,Karachi na Rawalpindi.

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan,Benazir Bhutto alierejea nyumbani mwezi wa Oktoba baada ya kuishi uhamishoni miaka minane iliyopita,amelaani hatua kali zilizochukuliwa na polisi na ametoa mwito wa kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa.Akaongezea kuwa anatazamia kuongoza maandamano dhidi ya Rais Musharraf na amri ya hali ya hatari iliyotangazwa na kiongozi huyo wa kijeshi.