1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ndayishimiye wa Burundi ziarani Kenya

Bruce Amani
31 Mei 2021

Mataifa ya Kenya na Burundi yamekubaliana kuimarisha sekta mbali mbali za kiuchumi na ushirikiano wa kimkakati baina yao, kufuatia ziara ya rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye nchini Kenya. 

https://p.dw.com/p/3uEOF
Bildkombo | Evariste Ndayishimiye und  Uhuru Kenyatta

Ndege iliyombeba rais wa Burundi Evariste Ndayeshimiye ilitua katika uwanja wa kimataifa wa Kisumu mwendo wa saa nne asubuhi, akiwa ameambatana na mke wake na na viongozi wengine, na kulakiwa na Afisa wa maswala ya maendeleo wa Umoja wa Afrika Raila Odinga kabla ya kupokelewa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ndogo ya rais jijini Kisumu.

Baada ya kukagua gwaride na kupigiwa mizinga 21 ya heshima, Marais hao na ujumbe wao walishiriki kikao cha faragha na muda mfupi baadae wakazungumza na waandishi habari ambapo wameweka wazi ushirikiano kati ya mataifa hayo kupitia makubaliano mbali mbali yaliyofikiwa.

Rais Uhuru Kenyatta amesema wamekubaliana kuendeleza ushirikiano ambao umekuwepo baina ya mataifa haya mawili kwa manufaa ya jumuiya ya Afrika Mashariki na Bara Afrika kwa ujumla huku wakifufua upya ushirikiano wa kimaendeleo uliotiwa saini mwaka 2018 na makubaliano mengine ya awali. "Katika maswala ya kimataifa tumetia msisitizo wa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi katika ngazi ya Umoja wa Mataifa kwa dhumuni la kufanikisha malengo ya Bara Afrika na maendeleo ya Kisumu".

Baadhi ya makubaliano ya ushirikiano yaliyotiwa saini ni katika sekta ya Kilimo cha ufugaji na uvuvi, uimarishaji huduma za umma kupitia mafunzo na ubadilishanaji ujuzi, ushirikiano wa maswala ya kisiasa, michezo, tamaduni na utalii, biashara na uwekezaji, elimu na makubaliano ya kudumisha ajenda ya maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika mwaka 2023. Rais Ndayishimiye ameelezea matumaini ya utekelezwaji wa makubaliano hayo kikamilifu. "Serikali ya Burundi inathamini ushirikiano kati ya mataifa yetu haya, tunatumai makubaliano yetu yatatekelezwa kikamilifu kwa mafao ya watu wa nchi hizi."

Marais hao baadae walishirikiana katika kuzindua miradi mbali mbali muhimu ikiwemo uzinduzi upya wa bandari ya Kisumu, ufunguzi wa shule ya elimu ya Uwanamaji miongoni mwa miradi mwingine.