1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatu Burundi

15 Februari 2015

Msemaji wa Rais Piere Nkurunziza wa Burundi amesema Jumapili (15.02.2015) kwamba kiongozi huyo atawania muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi wa mwezi wa Juni na kukaidi watu wanaosema atakiuka katiba.

https://p.dw.com/p/1Ec5Q
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.Picha: picture alliance/landov

Msemaji wa Rais Piere Nkurunziza wa Burundi amesema Jumapili (15.02.2015) kwamba kiongozi huyo atawania muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi wa Juni na kukaidi wanaharakati wanaosema kwamba hatua hiyo itakiuka katiba na kuhatarisha nchi hiyo kutumbukia kwenye ghasia.

Msemaji wake huyo Willy Nyamitwe amekaririwa akisema Nkurunzinza atagombea urais iwapo atachaguliwa kukiwakilisha chama chake cha CNDD-FDD katika kinyang'anyiro hicho "kwa kuzingatia katiba."

Tangazo hilo linakuja kufuatia kuzinduliwa kwa kampeni mapema mwezi huu na mashirika ya kijamii zaidi ya 300 nchini humo yakitowa wito kwa Nkuruzinza asigombee muhula huo wa tatu ili kuzuwiya kuzuka kwa ghasia nchini humo.

Kundi la mashirika hayo limemtaka rais huyo "kujifunza" kutokana na yale yaliyotokea nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambapo kulizuka maandamano ya maafa hapo mwezi wa Januari yaliosababishwa na hofu ya upinzani kwamba Rais Joseph Kabila alikuwa akijaribu kurefusha muda wake madarakani.

Watakaoandamana watashughulikiwa

Lakini Nyamitwe ameonya kwamba mtu yoyote yule anayejaribu kuchochea maandamano atakabiliwa na mkono wa sheria.Amesema "yoyote yule anayetowa wito kwa wananchi kuandamana mitaani ......atahesabika kuwa mfanya fujo na atashughulikiwa vilivyo."

Polisi wa Burundi wakiwa kazini.
Polisi wa Burundi wakiwa kazini.Picha: Esdras Ndikumana/AFP/Getty Images

Ameongeza kusema wananchi wa Burundi wanahitaji amani na haitokaa kimya pembeni katika kadhia kama hiyo.

Makundi ya haki za binaadamu yameonya juu ya kuongezeka kwa hofu kuhusiana na hatari ya kuzuka kwa ghasia kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo uliopangwa mwezi wa Juni wakati kukiwa na mfululizo wa mashambulizi ikiwa pamoja na mapigano ya siku tano mwezi uliopita kati ya jeshi la waasi.

Wanasiasa wa upinzani na wahakiki wanasema serikali inafanya kila iwezalo kuzima changamoto za kisiasa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo kwa kuwatia watu mbaroni,unyanyasaji na kukandamiza uhuru wa kutowa maoni.

Nia ya kun'gan'gania madaraka

Nkuruzinza alikuwa ameonyesha wazi kwamba alikuwa na nia ya kutumikia muhula wa tatu wa urais.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.Picha: I.Sanogo/AFP/GettyImages

Katiba ya Burundi inaruhusu tu rais wa nchi hiyo kuchaguliwa mara mbili kwa kipindi cha jumla cha miaka 10 madarakani lakini hoja anayoitumia Nkunrunzinza ni kwamba alikuwa amechaguliwa moja kwa moja na wananchi mara moja tu.

Katika muhula wake wa kwanza katika wadhifa huo wa urais mwanzoni mwaka mwaka 2005 alikuwa amechaguliwa na bunge la nchi hiyo.

Ni mwezi uliopita tu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon alitowa wito kwa viongozi wa Kiafrika wasi'ngan'ganie madaraka na waheshimu matakwa ya wananchi wao.

Nasaha za Ban zatupwa kapuni

Akizungumza katika Mkutano wa Kilele wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa Ethiopia Ban amesema watu duniani kote wanaelezea wasi wasi wao kuhusu viongozi wanaogoma kun'gatuka baada ya kumaliza muda wao madarakani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika Addis Baba Ethiopia(31.01.2015)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika Addis Baba Ethiopia(31.01.2015)Picha: picture-alliance/dpa/S. Kolli

Amewataka viongozi wote barani Afrika na duniani kwa jumla kuwasikiliza wananchi wao na kusema kwamba "viongozi wa kisasa hawastahiki kupuuza matakwa na matarajio ya wananchi wao."

Hapo mwezi wa Oktoba ghasia zilizuka nchini Ivory Coast wakati wabunge walipokuwa wakijiandaa kupiga kura ya kumruhusu kiongozi wa nchi hiyo Blaise Compaore mwenye umri wa miaka 63 ambaye alichukuwa madaraka hapo mwaka 1987 katika mapinduzi kugombania uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi wa Novemba 2015.Maandamano ya umma yalimlazimisha kujiuzulu.

Mapema mwezi huu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo takriban watu 42 waliuwawa katika maandamano ya kupinga kile kilichokuwa kikionekana kama jaribio la Rais Joseph Kabila kuendelea kun'gan'ania madaraka katika taifa ambalo ameliongoza kwa miaka 14.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.Picha: AFP/Getty Images/A. Wandimoyi

Nchi zikiwemo Benin,Congo- Brazaville na Rwanda zote zinasemekana kufanya mabadiliko ya katiba kuwawezesha viongozi wake wawanie muhula wa tatu madarakani.

Mataifa mengine ya Afrika ambapo sheria zimebadilishwa ili kuwanufaisha viongozi waliokuwa madarakani ni pamoja na Algeria,Angola, Chad,Djibouti na Uganda.

Burundi ni nchi ndogo isiokuwa na bahari ilioko Afrika ya Kati kwenye eneo la Nchi za Maziwa Makuu.

Hali ya kisiasa inaendelea kuwa ya mvutano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo wa bunge na urais hapo mwezi wa Mei na Juni.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Amina Abubakar