1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama atoa hotuba ya kukamilisha vita vya Iraq.

1 Septemba 2010

Wanajeshi 4,400 wa Marekani waliuawa, 34,260 walijeruhiwa na maelfu ya Wairaqi walikufa katika vita hivyo.

https://p.dw.com/p/P1aJ
Rais Obama alisema sasa ni wakati wa Wairaqi kulijenga taifa lao.Picha: AP

Rais wa Marekani alitangaza kukamilika kwa mashambulio ya Marekani nchini Iraq akisema lazima Wairaqi waamue mwelekeo wao kwa sababu Marekani inalenga kukabiliana na Al-Qaeda nchini Afghanistan na kujenga upya taifa lao. Rais Obama, akiyasema hayo katika hotuba yake jana, alisema Wamarekani wajitayarishe kwa umwagaji damu zaidi nchini Afghanistan na kwamba vita hivyo ni muhimu ili kuikinga Marekani kutokana na kitisho kikubwa cha Al-Qaeda.

Hotuba hiyo ya dakika kumi na nane ilimaanisha kuadhimisha wakati muhimu wa kujiondoa kwa Marekani kutoka Iraq, lakini ilizuia kutaja suala la ushindi au kushindwa,huku hali ya wasiwasi na ghasia ikilikumba taifa hilo ambalo Marekani ililivamia mwaka wa 2003.

Akizungumza kutoka katika ofisi yake kuu katika ikulu ya Marekani, Rais Obama, ambaye alitumia wakati wake wa kampeni ya urais kupinga vita vya Iraq, alizungumzia fahari yake juu ya kujitolea kwa wanajeshi wa vikosi vya Marekani na alitoa wito wa uzalendo ili kuliwaza mgawanyiko uliosababishwa na vita hivyo.

Irak Anschläge
Rais Obama alisema viongozi wanafaa kuunda serikali ya kudumu kwa haraka nchini Iraq.Picha: AP

Akiwa katika sehemu aliyokuwa rais wa zamani, George Bush aliyetangaza vita dhidi ya Iraq miaka saba iliyopita, Bw Obama alisema operesheni ya kuipa Iraq uhuru imekamilika na Wairaqi sasa wana jukumu la usalama wa taifa lao.

Licha ya mzozo wa kisiasa nchini Marekani, Rais Obama alijaribu kuwakumbusha Wamarekani kuhusu umuhimu wa kuufufua uchumi wa Marekani, huku kuimarika huko kwa polepole kukididimiza umaarufu wake na kuna kitisho kwa Wademocrat katika uchaguzi wa ubunge wa mwezi Novemba wakapoteza viti. Alisema kwamba Wamarekani wamekalimilisha wajibu wao nchini Iraq na sasa wanafaa kulijenga upya taifa lao, kwamba kukamilisha vita hivyo sio kwa maslahi ya Iraq pekee bali ni kwa manufaa ya Wamarekani.

Rais Obama alitaja kwamba Marekani imejitolea kuweka mustakabali wa Iraq katika mikono ya watu wake. Waliwatuma wanajeshi wao kujitolea nchini Iraq na wametumia raslimali nyingi nje wakati wa bajeti finyu nyumbani. Alisema wamevumilia kwa sababu ya imani walionayo na watu wa Iraq, imani kwamba kutoka katika majivu ya vita, mwanzo mpya utazaliwa kutoka katika chanzo cha ustaarabu. Alisema sasa ni wakati wa mabadiliko mapya.

Irak / USA / US-Soldat
Wanajeshi wapatao 50,000 watasalia nchini Iraq kutoa mafunzo na kukabiliana na Al-Qaeda hadi mwishoni mwa 2011.Picha: AP

Rais Obama aliapa kuviondoa vikosi vya Marekani kutoka Iraq na tayari amewaondoa kiasi ya wanajeshi laki moja huku akiimarisha vita nchini Afghanistan. Hata hivyo, huku wanajeshi elfu hamsini wakisalia nchini humo kutoa mafunzo na kuendesha shughuli dhidi ya ugaidi hadi mwisho wa mwaka ujao, alionya kwamba mashambulio ya wanajeshi wa Marekani yameisha na ghasia hazitakithiri. Alisema kwamba wapiganaji wataendelea kuripua mabomu wakiwashambulia Wairaqi na kuchochea wasiwasi wa kidini lakini alisisitiza kwamba Wairaqi hawatawaruhusu magaidi kuvuruga hatima yao.

Kiasi ya wanajeshi 4,400 wa Marekani waliuawa katika vita hivyo, wengine 34,260 walijeruhiwa, raslimali nyingi imetumiwa licha ya mzozo wa kiuchumi na maelfu ya Wairaqi walikufa. Alitoa mwito kwa viongozi nchini Iraq kuunda serikali ya pamoja kwa haraka ambayo itawawakilisha na kuwajibika kwa raia. Waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, alisema ni siku itakayosalia katika kumbukumbu ya Wairaqi kwamba ni taifa lenye mamlaka na uhuru.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Othman Miraji