1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Putin yupo ziarani nchini China

Amina Mjahid
8 Juni 2018

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili nchini China na kukutana na rais Xi Jinping katika ziara ya siku tatu inayonuiwa kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi kwa nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/2z8ou
Russischer Präsident Putin mit chinesischem Präsdient Xi Jinping
Picha: Reuters/J. Lee

Rais wa China Xi Jinping alimkaribisha rais Putin kwa gwaride la heshima katika ukumbi wa kitaifa mjini Beijing. Viongozi hao ambao wote hawakualikwa katika mkutano wa kilele wa mataifa saba yalioimara kiuchumi G7, utakaofanyika nchini Canada Ijumaa (08.06.18) na Jumamosi (09.06.18) wanatarajiwa kutia saini makubaliano ya kibiashara baadaye hii leo.

Badaa ya kukaribishwa rasmi nchini humo Putin alikutana pia na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang kabla ya kuwa na mazungumzo rasmi na rais Xi. Putin alimwambia Li kwamba biashara kati ya Urusi na China pamoja na mahusiano ya kiuchumi yamefana na wanatafuta sehemu nyengine ya ushirikiano.

Li kwa upande wake amesema biashara kati yao inatarajiwa kufikia dola bilioni 100 mwaka huu  huku akisema kuwa China iko tayari kabisa kupanua ushirikiano katika Nyanja mpya ikiwa ni pamoja na nishati ya nyuklia.

APEC  Wladimir Putin und Xi Jinping
Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa China Xi Jinping Picha: picture-alliance/dpa/K.Zavrajin

Urusi imelazimika kuimarisha uhusiano wake na Asia baada ya uhusiano wake na nchi za Magharibi kuingia doa

Awali katika mahojiano yaliyofanywa na chombo kimoja cha habari cha China, Putin alisema Urusi na China wana nia ya kuimarisha ushirikiano wao katika maeneo kama miundo mbinu, nishati utafiti wa kisayansi na masuala ya teknolojia ya hali ya juu.

Urusi imelazimika kuimarisha mahusiano yake na Asia katika miaka ya hivi karibuni baada ya uhusiano wake na mataiafa ya Magharibi kuingia doa kutokana na mgogoro wa Ukraine.

Kando na hayo Putin katika ziara yake hiyo ya siku tatu nchini China anatarajiwa kulihutubia shirika la ushirikiano la Shanghai SCO ambalo ni kanda ya ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi linalochangia kuboresha uhusiano kati ya Urusi na china. Mkutano wa kilele wa shirika hilo utafanyika katika mji wa china wa Qingdao mwishoni mwa juma hili.

Putin amemuelezea Xi kuwa mtu anayeaminika. Xi ndio rais wa hivi karibuni pekee ambaye rais Putin alisherehekea naye siku yake yake kuzaliwa. Urusi imeendelea kuitegemea China kama soko kwa uuzaji wa bidhaa zake za nishati kama njia moja ya uwekezaji katika miradi ya miundo mbinu.

Ziara hii ni ya kwanza tangu Putin aliponza hatamu yake mpya kama rais wa Urusi  mwenzi mmoja uliyopita.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AP

Mhariri: Gakuba, Daniel