1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Puttin atoa hotuba ya mwisho kabla ya kung'atuka mamlakani

26 Aprili 2007

Rais Vladmir Puttin amelihutubia bunge la Kremlin katika hotuba yake ya mwisho kama rais wa Urusi.

https://p.dw.com/p/CHFN
Rais Vladmir Puttin wa Urusi
Rais Vladmir Puttin wa UrusiPicha: AP

Rais Vladmir Puttin mwenye msimamo wa ukakamavu hasa pale kunapojitokeza mtu anaeukosoa utawala wake, katika hotuba yake leo hii mbele ya bunge la Kremlin ametaja kuwa wageni wanajaribu kuingilia kati maswala ya ndani ya nchi yake.

Amesema kuwa makundi hayo yana nia ya kupora utajiri uliopo nchini mwake na wakati huo huo kuwanyang’anya warusi uhuru wao wa kiuchumi na vilevile uhuru wa kisiasa.

Maafisa wa Urusi katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakilalamika kuwa nchi za magharibi zinajiingiza katika mambo ya kisiasa ya nchini Urusi kwa kuyafadhili kifedha mashirika yanayodai kuwa yanatetea demokrasia, rais Puttin amesema pesa zinazotoka nchi za nje zinazidi kuoengezeka, na kwa kutumia pesa hizo watu wanajiingiza katika mambo ya ndani ya Urusi.

Katika hotuba yake kwa taifa ambayo ameitaja kuwa ni ya mwisho katika wadhfa anaoshikilia wa rais wa Urusi, Puttin amesema wazi kuwa hana nia ya kugombea awamu ya tatu ya urais lakini wakati huo huo hakutaka kumtaja yule ambae atakuwa mrithi wake na wala hakuashiria chochote ambacho labda kingeleta shauku kuwa huenda anataka kuyadhibiti mamlaka nyuma ya pazia.

Katika hotuba yake rais Puttin amekumbushia kuwa nchi yake inaingia katika msimu wa siasa kwani uchaguzi wa bunge nchini Urusi unatarajiwa kufanyika mwezi Desemba na kisha kufuatiwa na ule wa rais mwezi Machi mwakani.

Rais Vladmir Puttin ameonya kwamba ataendeleza pingamizi yake dhidi ya mpango wa Marekani wa kuwekeza makombora ya ulinzi katika bara Ulaya.

Rais wa Urusi amezilaumu nchi za jumuiya ya NATO kwa kutoheshimu mkataba wa mwaka 1990 unao dhibiti hatua za kupeleka majeshi ya kawaida katika sehemu mbali mbali za ulimwengu.

Vladmir Puttin amesema namnuku - “Wenzetu wanaitumia hali iliopo sasa kuongeza kambi za kijeshi pamoja na vifaa karibu na mipaka yetu’’ - mwisho wa kumnukuu.

Matamshi hayo ya rais Puttin katika hotuba yake yametokezea muda mchache tu kabla ya wajumbe wa NATO na wenzao wa Urusi walipokuwa wanajiandaa kuanza mazungumzo ambayo waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice ameyataja kuwa sio tishio kwa Urusi na hivyo basi kuliita wazo la rais Puttin kuwa ni la mzaha.

Katibu mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer amesema atamtaka waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov aeleze nia na uamuzi wa rais Puttin juu ya kutaka kuusimamisha mkataba wa mwaka 90 kuhusu majeshi ya kawaida na wakati huo huo amekanusha madai ya rais Puttin kwamba NATO inaupuuza mkataba huo.