1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Santos wa Angola atuhumiwa

26 Oktoba 2016

Mahakama ya juu ya nchini Angola imemuagiza rais wa nchi hiyo, Jose eduardo dos Santos kujibu tuhuma kuhusu sababu za kumteua binti yake Isabel dos Santos kuongoza kampuni ya taifa ya mafuta ya Sonangol.

https://p.dw.com/p/2RiTY
Präsidentschaftskandidat Jose Eduardo dos Santos Angola
Picha: picture-alliance/dpa

Dos Santos alimteua binti yake huyo Bilionea kama mtendaji mkuu wa kampuni hiyo a taifa ya mafuta ya Sonangol mnamo mwezi Juni mwaka huu, na mara baada ya uteuzi mwanamama huyo aliahidi kuifanyia mabadiliko makubwa kampuni hiyo kiutendaji na kiuzalishaji ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kukabiliana na matokeo ya kukatisha tamaa kwenye bei ya mafuta.

Kulingana na nyaraka za mahakama hiyo ya juu ambazo shirika la habari la Reuters limepata naka zake, rais Eduardo Santos ametakiwa kujibu tuhuma hizo. Mahakama hiyo imeanza kuyafanyia kazi maombi ya shauri lililowasilishwa mahakamani hapo na wanasheria 14 wa Angola wanaomtuhumu rais kwa kuendekeza undugu na kuvunja sheria ya uaminifu ya nchi hiyo.

Hata hivyo, si rais mwenyewe, msemaji kutoka kitengo cha mawasiliano cha Ikulu ama Isabel mwenyewe hawakupatikana mapema wala kupokea simu kuzungumzia kuhusu mwito huo wa mahakama. Isabel, aliteuliwa kuchukua mamlaka hayo mara baada ya hatua ya kushtukiza ya rais ya kuvunja bodi ya Sonangol.

Miongoni mwa hatua ambazo Isabel aliahidi kuzichukua dhidi ya kampuni hiyo ni pamoja na kuigawanya kampuni hiyo na kuwa na vitengo vitatu, ambavyo kimoja kitaangazia zaidi masuala ya uzalishaji, kitengo cha usafirishaji na vifaa na kitengo kitakachohusika na mikataba. 

Isabel dos Santos - Unternehmerin Tochter des Präsidenten von Angola
Binti wa Rais Santos, Isabel dos Santos, ambaye ni mtendaji mkuu wa Sonangol.Picha: Nélio dos Santos

Uteuzi huo ulichukuliwa na baadhi ya wachambuzi kama hatua ya rais dos Santos ya kujitengenezea njia ya urithi kwa ukoo wake, iwapo atatekeleza azma yake aliyotangza mwezi Machi ya kuondoka madarakani ifikapo mwaka 2018, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu, ingawa wengine wanasema inawezekana alikuwa akimaanisha kuleta mabadiliko ndani ya kampuni hiyo. 

Angola, ambayo ni mwanachama wa muungano wa nchi zinazosafirisha mafuta nje, OPEC, kwa sasa ni mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta barani Afrika, baada ya Nigeria kuanguka kiuzalishaji kutokana na mashambulizi ya wanamgabo dhidi ya miudombinu ya mafuta na matatizo mengine. Hata hivyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuanguka kwa bei ya mafuta, hatua iliyoifanya nchi hiyo kupunguza matumizi. 

Isabel Santos, ambaye ni binti wa kwanza wa Rais santos, ametajwa kwenye jarida la FORBES kama mwanamke tajiri zaidi barani Afrika, ambaye pamoja na sasa kuwa mtendaji mkuu kwenye kampuni hiyo ya taifa ya mafuta, bado amewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta za mawasiliano, benki, televisheni ya setilaiti na hata kwenye michezo. Utajiri wake unafikia Dola za kimarekani, Bilioni 3.2.

Afrika Angola Sonangol in Luanda
Kampuni ya Sonangol, iliyoko mjini Luanda, Angola.Picha: DW/P. Borralho

Mwandishi wa habari Rafael Marques wa Angola ambaye amekuwa akifuatilia mzizi wa utajiri wa Isabel kwa miaka mingi anasema kwamba baba yake Jose Eduardo dos Santos amekuwa na dhima kubwa katika kumjengea utajiri huo. Ameiambi DW kwamba kila alichotaka Isabel baba yake alihakikisha anakipata. Anasema, aliwahi hata kumpa madaraka ya kusimamia fedha katika mikataba mikubwa ya serikali, ingawa Isabel mwenyewe anapinga tuhuma hizo.
  
Hata hivyo, baadhi ya watu wanamuangalia Isabel Dos Santos kama mfano wa wafanyabiashara barani Afrika ambao wametoa nafasi za ajira zinazohitajika kwa kiasi kikubwa, katika taifa hilo ambalo asilimia 24 ya watu hawana kazi, hii ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014. 

Mwandishi: Lilian Mtono/http://www.dw.com/sw/utajiri-wa-binti-wa-rais-wa-angola/a-36152195/Rtre.
Mhariri: Iddi SSessanga