1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sarkozy akamilisha ziara yake nchini Afghanistan

22 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CfEZ

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, ameondoka nchini Afghanistan kuelekea Tajikistan, baada ya kufanya ziara fupi mjini Kabul.

Kiongozi huyo amekutana na rais wa Afghanistan, Hamid Karzai na baadhi ya wanajeshi wa Ufaransa wanaohudumu nchini humo wakiwa sehemu ya kikosi cha jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi, NATO.

Akizungumza baada ya mkutano wake na rais Karzai, rais Sarkozy amesema jumuiya ya kimataifa haipaswi kukubali kushindwa katika vita dhidi ya ugaidi nchini Afghanistan.

Aidha kiongozi huyo ameitolea mwito Pakistan iongeze juhudi za kupambanana na ugaidi katika eneo hilo. Ufaransa huenda iongeze idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan.

Wakati huo huo, waziri mkuu wa Australia, Kelvin Ruud, amezuru Afghanistan katika ziara ambayo haikutangazwa. Bwana Ruud amekutana na rais Karzai mjini Kabul na kufanya mkutano na waandishi wa habari ulioonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni ya kitaifa.

Kelvin Ruud amewatembelea wanajeshi wa Australia walio katika mkoa wa Uruzgan kabla kuwasili mjini Kabul.