1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sarkozy wa Ufaransa na Kansela Merkel wa Ujerumani washauriana leo

16 Agosti 2011

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa leo watakutana mjini Paris

https://p.dw.com/p/12H8r
Rais Sarkozy wa Ufaransa na Kansela Merkel wa Ujerumani wanashauriana juu ya mzozo wa madeni katika eneo la sarafu ya EuroPicha: AP

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa leo watakutana mjini Paris kushauriana juu ya hatua zitakazochukuliwa ili kuleta hali ya utulivu wa kifedha katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro. Hasa watazungumzia juu ya mikakati thabiti ya kukabiliana na mizozo, na namna ya kuziongoza siasa za kiuchumi. 

Matarajio ya mkutano huu baina ya Ujerumani na Ufaransa ni makubwa. Ni makubwa mno hata mtu aliweza kugundua alama zake katika soko la hisa la mjini Paris kutokana na tamko dogo alilotoa jana msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert. Lilikuwa suala kama Angela Merkel na  Nicolas Sarkozy pia watazungumzia mada inayobishiwa ya kutolewa hati za dhamana za mikopo kwa sarafu ya Euro. Steffen Seibert alisema suala hilo halitazungumziwa. Nusu saa baadae bei za hisa za makampuni katika soko la Paris la CAC zilianguka, na soko hilo likapata hasara.

Symbolbild 50 Euro 500
Nchi za sarafu ya Euro ziko katika mbinyo wa kutanzua mzozo wa madeni. Picha hiyo ni noti ya Euro 50Picha: Gravicapa/Fotolia

Sio tu nchi zilizo katika mzozo wa kifedha, kama vile Ugiriki na Utaliana, zinazoweka mataumainio yao katika hati hizo za dhamana za Euro. Mara kadhaa wafanyabiashara wametaka zianzishwe dhamana hizo za kukopesha. Lakini hadi sasa sio Angela Merkel wala Nicolas Sarkozy waliovutiuwa na fikra hiyo. Kama wataweza kuhimili mbinyo wa kutoka kwenye masoko ni jambo ambalo halijulikani kabisa hadi sasa. Waziri wa uchumi wa Ufaransa, Francois Baroin, hata hivyo, ana hakika kwamba Ufaransa itaweza kuukiuka mzozo wa sasa:

"Siwasikilizi kabisa- sio leo, sio jana au kesho- watume wa majanga. Sisi tuna dhamana. Kuna njia za kiufundi, kuna maamuzi ya kisiasa. Jambo hilo tunaliamini, na litafanya kazi."

Waziri Baroin anakusudia, kwa mfano, kupiga marufu ulanguzi wa dhamana za mikopo, jambo ambalo Ufaransa ililizungumzia wiki iliopita. Ulanguzi huo wa hali ya juu wa pata potea hivi sasa unakatazwa katika nchi sita za Umoja wa Ulaya, ikiwemo Ujerumani. Kila nchi nyingi zaidi zikijiunga na marufuku hiyo, ndipo jambo hilo litakapofanya kazi zaidi.

"Kununuliwa hati hizo za mikopo kwa dhamana hewa, mtu anaweza kupata fedha nyingi katika kipindi cha muda mfupi, bila ya hata kumiliki hisa zenyewe. Biashara ya aina hiyo mtu lazima aiwekee vikwazo."

Hivyo ndivyo anavosema waziri wa uchumi wa Ufaransa. Pia suala la kuweko uwiano ulio bora katika siasa ya uchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya litakuwemo katika ajenda ya mazungumzo ya leo baina ya Kansela Merkel na Rais Sarkozy. Wote wawili wanataka kuepusha kwamba katika wakati ambapo masoko ya fedha yanaguswa na hata mambo madogo kabisa, kusitolewe habari kutoka makao makuu ya Umoja wa Ulaya ambayo yataongeza vuguvugu katika masoko ya hisa.

Kwa rais wa Ufaransa, mkutano huu utakuwa na umuhimu mwengine kabisa. Kama amemwita Kansela Merkel aende Ufaransa ili kwa pamoja wazungumzie juu ya mzozo wa sarafu ya Euro ni pia risala kwa wananchi wake. Wananchi hao wanatakiwa washuhudie kwamba  Sarkozy, kupitia nguvu za kivitendo, anayadhibiti masuala ya uchumi. Kwani kwa hivi sasa katika kila Wafaransa watatu, basi mmoja anaamini kwamba Sarkozy anaweza kuudhibiti mzozo mpya. Na kutokana na uchunguzi wa karibuni wa maoni ya wananchi ni kwamba Wafaransa  hasa wana imani na Kansela Angela Merkel.

Mwandishi: Junghans, Daniela/ Othman, Miraji/ ZR

Mhariri. Mohammed Abdulrahman