1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump avutana na vyombo vya habari

Sudi Mnette
23 Januari 2017

Rais Donald Trump ameanza juma la kwanza la majukumu yake ya urais huku akiwa katika vita vya maneno na vyombo vya habari jambo linalozusha swali ni kwa kiwango gani taarifa za Ikulu zinaweza kuwa za kuaminika.

https://p.dw.com/p/2WF4E
US Präsident Donald Trump spricht zur Vereidigung weiterer Minister
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Picture-Alliance/dpa/A. Harnik

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sean Spicer leo ataitisha, mkutano wa kwanza wa waandishi habari, ambapo atakabiliwa na maswali kuhusu kauli ya Jumamosi usiku pamoja na udanganyifu wa kuongeza idadi ya watu katika hafla ya kuapishwa kwa Trump, pamoja na ahadi ya utawala huo mpya kuwa utaviwajibisha vyombo vya habari.

Baadhi ya wafuasi wa Trump, bila shaka wameendelea na uhasama na vyombo vya habari kwa kile wanachokiona kwamba viliingilia kampeni ya urais. Lakini sasa vigingi vimeongezeka zaidi.

Utata wa taarifa

Spicer alitoa taarifa mbili zisizo na uthibitisho katika mikutano yake, kwanza ikiwe ile ya wapiga picha katika hafla ya kupishwa kwa Rais Trump walikuwa na lengo la makusudi kuonesha idadi ndogo ya wanaomuunga mkono kiongozi huyo, na baadae kwa upande wa Trump kukaoneshwa picha zenye idadi kubwa ya watu.

Inauguration Obama vs Trump
Utata wa idadi ya watu walioudhuria kuapishwa kwa Obama ikilinganisha na TrumpPicha: picture-alliance/AP Photo

Lakini mikanda ya video zilizorekodiwa zilionesha tofauti ya idadi ya watu iliyokuwepo wakati Rais wa awamu iliyopita Barack Obama akiapishwa na Ijumaa, alivyoapishwa Trump. Mikanda hiyo ya video ilionesha kwa mara ya kwanza eneo la wafuasi  likiwa na uwazi.

Lakini pia tofauti yake na waandishi habari Trump alionesha katika mkutano wake wa kwanza na waandishi habari baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani Januari 11. Kutokana na tuhuma za mahusiano yake na Urusi, kiongozi huyo na timu yake waliyalaani mashirika ya habari kama CNN na Buzz Feed na baadae kukataa kujibu swali la mwandishi wa CNN.

Matarajio ya China

Aidha China imeutaka utawala la Trump kushiriki katika kutaka kuitambua "China Moja". Waziri wa mambo ya Kigeni wa China Hua Chunying anasema."Tunautaka utawala wa Marekani, kuelewa kwa ukamilifu unyeti wa suala la Taiwan na kuendelea katika kufanikisha sera ya China moja".

Katika hatua nyingine, kundi la Hamas la Palestina, limemuonya Rais Trump kufuatia kile walichokiita hatari ya ahadi yake ya kuhamisha ubalozi wa Marekani katika eneo la walowezi la Jerusalem. Katika taarifa yake kundi hilo lenye kuidhibiti Gaza tangu 2007 limesema Marekani imevuka msitari mwekundu na inaongeza utata katika  mchakato wa amani  kati ya Israel na Palestina.

Kauli hiyo ya Hamas imetolewa baada ya Rais Trump kuzungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa njia ya simu ambapo pamoja na suala hilo, walijadili mahusiano kati ya nchi hizo mbili na vitisho kutoka kwa Iran. Aidha Trump amemwalika Netanyahu kuitembelea Ikulu ya White House mwezi ujao wa Februari.

Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman