1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Benki ya Duniani ziarani DRC

10 Agosti 2009

Rais wa Benki ya Dunia Robert Zoellick yukomjini Kinshasa tangu jana usiku kwa ziara ya siku tatu katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

https://p.dw.com/p/J78e
Rais wa Benki ya Dunia Robert ZoellickPicha: picture-alliance/ dpa

Rais huyo wa Benki pamoja na masuala mengine atajaribu kuchagiza kufanyiwa mabadiliko mkataba ulifikiwa kati ya China na nchi hiyo wenye thamani ya dola billioni 9.

Akizungumza  hapo mapema  alipokua  njiani kuelekea nchini humo, amesema kuna hali ya kufikiwa kwa makubaliano hayo ya kuurekebisha mkataba huo, ambao Shirika la Fedha duniani IMF limekuwa na wasi wasi nao.

IMF  inahofu kuwa  mkataba huo ambao unatumia akiba ya madini ya Kongo kama dhamana ya ujenzi wa miundo mbinu utakaofanywa na China, unaweza kuitumbukiza nchi hiyo katika deni kubwa.

Wasi wasi huo umelifanya shirika hilo kuchelewa kutoa msamaha wa deni la thamani dola billioni 10 ambalo linaidai nchi hiyo.Lakini Bwana Zoellick amesema kuwa kuna hatua iliyofikiwa katika kuuangalia upya mkataba huo.

Amesema taarifa ambazo wamezipata ni kwamba kampuni la kichina limesema liko tayari kurekebisha aina ya dhamana kutoka ile ya zamani ya uchimbaji madini na kuwa nyingine, hali ambayo rais huyo wa Benki ya Dunia amesema kama hatua hiyo itafikiwa basi wataendelea na mpango wa kuisamehe deni hilo.

Maafisa wa China waliyoko mjini Kinshasa mpaka sasa hawajuzungumza lolote kuhusiana na  hatua hiyo.Kwa upande wao maafisa wa serikali ya Kinshasa wamesema mkataba huo waliyofikia na China hauwezi kuitumbukiza nchi hiyo katika deni lolote.

Wamesisitiza kuwa mradi huo ujenzi wa miundo mbinu ni muhimu kwa nchi hiyo, ambayo imeharibika kutokana na miongo kadhaa ya utawala wa kidikteta pamoja na vita  vya kuanzia mwaka 1998 hadi 2003.

Hapo mwezi Mei wakati wa ziara yake nchini humo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo la IMF Dominique Strauss-Kahn alisema kuwa tatizo bado lipo na kwamba hawawezi kuchukua uamuzi wa kuifutia madeni.

Rais wa Benki ya Dunia yuko nchini Kongo kutathmini jinsi nchi hiyo inavyojaribu kukabiliana na  madhara ya kuyumba kwa uchumi wa dunia na kwa vipi benki  hiyo ya dunia inaweza kuisaidia.

Kesho Bwana Zoellick anatarajiwa kwenda Mashariki mwa Kongo kukutana na Rais Joseph Kabila ambaye kwa muda wa wiki moja sasa yuko katika eneo  hilo.

Eneo hilo la Mashariki mwa Kongo kilikua kitovu cha mapigano ya miaka kadhaa kati ya  majeshi ya serikali na makundi ya waasi wa kikongomani pamoja na  masalia ya wapiganaji wa  kihutu wa kundi la FLDR kutoka nchi jirani ya Rwanda.

Baadhi ya wapiganaji hao wanasemekana walihusika katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda 1994 kabla ya kukimbilia Kongo baada ya wapiganaji wa RPF wakiongozwa na  rais wa sasa Paul Kagame kutwaa madaraka.

Präsident Joseph Kabila und Präsident Paul Kagame 2004
Rais, Joseph Kabila wa Kongo na Rais Paul Kagame wa RwandaPicha: AP
Wiki iliyopita, marais Kabila na Kagame walikutana mjini  Goma kuzungumzia  masuala muhimu yanayozihusu nchi zao mbili.

Mwandishi: Aboubakary Liongo/Reuters

Mhariri.M.Abdul-Rahman◄