1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabolivia wapiga kura ya hapana katika mabadiliko ya Katiba

Mjahida 24 Februari 2016

Rais wa Bolivia Evo Morales ameshindwa katika hatua yake ya kutaka kuendelea kuongoza muhula wa nne madarakani, hii ikiwa ni mara yake ya kwanza kushindwa tangu aingie uongozini mwaka wa 2006.

https://p.dw.com/p/1I10B
Bolivien Referendum Verfassungsreform Evo Morales
Rais Evo Morales wa BoliviaPicha: Getty Images/AFP/A. Raldes

Morales ameamua kuheshimu matokeo rasmi ya kura juu ya mabadiliko ya katiba katika mchakato uliofanyika jumapili, hatua iliyotarajiwa kurefusha utawala wake hadi miaka 19. Muhula wa Morales unamalizika rasmi mwaka wa 2020.

Raisi wa tume ya uchaguzi Katia Uriona amesema Kura Jumla zilizohesabiwa ni asilimia 99.72. na asilimia 51.3 walipiga kura ya hapana katika kura hiyo ya maoni huku asilimia 48.7 wakipiga kura ya ndio. Morales awali alisisitiza kusubiri matokeo kamili kujumuishwa kutoka maeneo ya mashinani ambako ana ungwa mkono kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo wafuasi wa upinzani walifurahishwa na matokeo ya kura hiyo na kuanza kusherehekea mjini La Paz na katika maeneo yasiyomuunga mkono Morales kama Potosi na Santa Cruz.

Bolivien Referendum Verfassungsreform Evo Morales Protest
Raia wa Bolivia wakati walipokuwa wanasubiri matokeo ya kura ya maoniPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Karita

Morales, aliye na miaka 56 amekuwa uongozini kwa muongo mmoja, akipata uungwaji mkono wa makundi ya wazalendo wa Bolivia na matawi ya watu wa vijijini katika moja ya nchi masikini katika bara la Amerika.

Matokeo huenda yakampa changamoto Morales katika muhula wake uliyobakia

"Leo taifa limegawanyika, lakini ni kwa muda tu, hatua ya kusawazisha hilo itatokana na Morales mwenyewe, chama chake, na makundi ya upinzani kutafuta njia ya kufanya kazi pamoja," alisema mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini humo Carlos Cordero.

Awali upinzani ulikuwa na hofu kuwa serikali ilipanga kubadilisha matokeo hayo. "Tumejipatia tena demokrasia na Uhuru wa kuchagua," alisema Samuel Doria Medina, aliyewahi kushindwa mara mbili na Morales katika uchaguzi wa rais.

Rais huyo wa Bolivia Evo Morales amesema amekuwa akijitayarisha kutogombea muhula wa nne iwapo wapiga kura watakataa mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maoni.

Bolivien Referendum Verfassungsreform Evo Morales
Ujumbe uliandokwa mtaani Bolivia unaoonesha hapana kwa Hatua ya Morales ya kurefusha muhula wake madarakani.Picha: Getty Images/AFP/A. Raldes

Tangu alipochukua madaraka amechaguliwa tena mara mbili na amefanikiwa kuinua uchumi wa nchi hiyo yenye utajiri wa madini na gesi. Lakini wapinzani wamemshutumu kuhusika katika masuala ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha.

Huku hayo yakiarifiwa wanaharakati wanasema matokeo ya kura ya maoni yanaweza kuvuruga muda wake uliyobakia madarakani, na kusababisha mivutano ya ndani kwa ndani ya kutaka kumrithi. Andres Torres anasema hatua hiyo inaweza kukidhoofisha chama chake na kuleta mgogoro na matatizo makubwa katika juhudi zake za kuelekea katika usoshalisti.

Mwandishi: Amina Abubakar AFP/Reuters

Mhariri: Saumu Yusuf