1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raisi aapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya Qassem Soleimani

Tatu Karema
3 Januari 2022

Rais wa Iran Ebrahim Raisi ameapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya jenerali Qassem Soleimani aliyeuawa 2020, iwapo Donald Trump hatotashtakiwa kwa kosa la jinai la mauaji ya jenerali huyo

https://p.dw.com/p/455WV
Ebrahim Raisi‚
Picha: Iranian Presidency/Handout/AA/picture alliance

Katika taarifa aliyotoa leo kupitia televisheni, Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema ikiwa Trump na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo hawatashtakiwa kwa tukio hilo la uhalifu la mauaji ya Soleimani, waislamu watachukuwa hatua za kisasi kulipiza kifo hicho cha kiongozi huyo aliyemtaja kuwa shaheed. Soleimani aliuawa nchini Iraq katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani lililoagizwa na Trump.

Wakati huo huo, ndege mbili zisizo na rubani zimedunguliwa katika uwanja wa ndege wa Baghdad hatua inayotajwa na afisa mmoja wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa kwamba inasadifiana na kumbukumbu ya mauaji ya Soleiman. Hakuna ripoti za uharibifu wala majeruhi iliyotolewa kuhusiana na kisa hicho ambacho pia kimethibitishwa na afisa mmoja wa usalama wa Iraq.

USA I Ex-Präsident Donald Trump
Donald Trump - Aliyekuwa rais wa MarekaniPicha: The Right View/ZUMA/picture alliance

Afisa huyo anayeshirikiana na muungano wa jeshi la kimataifa unaoongozwa na Marekani katika kukabiliana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, ameliambia shirika la habari la AP kwamba mfumo wa ulinzi wa C-RAM katika katika kituo cha msaada wa kidiplomasia kilinasa ndege hizo mbili zisizo na rubani. Mfumo wa C-RAM hulinda mitambo ya Marekani nchini Iraq. Afisa huyo ameongeza kuwa hilo lilikuwa shambulizi hatari sana dhidi ya uwanja wa ndege wa kiraia. Hakuna kundi lililokiri mara moja kuhusika na shambulio hilo ijapokuwa mbawa moja ya ndege hizo ilikuwa imeandikwa ''kisasi cha Soleiman huku nyingine ikiandikwa``operesheni za kisasi kwa viongozi wetu.

Waasi wa Houthi waiteka nyara meli ya bendera ya UAE

Huku hayo yakijiri, Waasi wa Houthi wanaodhibiti sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen leo wameiteka nyara meli moja ya mizigo iliyokuwa inapeperusha bendera ya Falme za kiarabu kwenye bahari ya sham karibu na mji wa bandari ya Hodeidah nchini Yemen. Kituo cha televisheni cha Al-Arabiya kimesema taarifa ya kutekwa kwa meli hiyo imetolewa na muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia. Utekaji nyara huo ni ishara ya karibuni zaidi ya mvutano katika Mashariki ya Kati huku wadukuzi wakilenga tovuti moja kuu ya gazeti la Jerusalem post kuadhimisha mauaji hayo ya Soleimani.