1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Iran Hassan Rouhani aizuru Urusi

Caro Robi
28 Machi 2017

Rais wa Urusi Vladimir Putin anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Iran, Hassan Rouhani yatakayofuatiliwa kwa karibu kuhusu hatua watakayochukua kuhusu mzozo wa Syria. Kiongozi huyo wa Iran yuko ziarani mjini Moscow.

https://p.dw.com/p/2a6cI
Kombobild Hassan Rouhani und Wladimir Putin
Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Korotayev/TASS/dpa/M. Klimentyev

Ziara hiyo rasmi ya kwanza ya Rais Hasaan Rouhani nchini Urusi inakuja wakati pande zinazozana nchini Syria zikijaribu kutafuta njia za kuvimaliza vita ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka sita huku nchi hizo mbili, Urusi na Iran zikijaribu kuitenga Marekani kuwa na ushawishi mkubwa katika mazungumzo ya kutafuta amani Syria.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bahram Ghasemi amesema kuwa viongozi hao wawili watajadili masuala ya kikanda, hasa mzozo wa Syria na suluhisho za kuumaliza haraka mzozo huo pamoja na masuala ya kukabiliana na ugaidi na itikadi kali.

Kulingana na kituo cha televisheni cha serikali ya Iran, Rais Rouhani anaandamana na Waziri wa mambo ya nje Javad Zarif, waziri wa mafuta Bijan Zananeh na maafisa wengine wa ngazi ya juu katika ziara hiyo ya Urusi.

Urusi na Iran ndiyo washirika wakuu wa Assad

Zarif ameliambia Shirika la habari la Reuters kuwa Urusi inaweza kutumia kambi zake za kijeshi kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambo nchini Syria.

Russland Syrien Assad bei Putin
Rais wa Syria Bashar al Assad na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/RIA Novosti/Kremlin/A. Druzhinin

Anatarajiwa kutia saini makubaliano kadhaa ya ushirikiano wa kiuchumi na Urusi. Ikulu ya Rais wa Urusi ya Kremlin imesema ziara hiyo ya Rouhani nchini humo itaangazia uwezekano wa kutanua biashara, uchumi na uwekezaji.

Baada ya kuwasili jana mjini Moscow, Rais Rouhani alikutana na Waziri mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev na kusema anatumai ziara yake itaanzisha ukurasa mpya wa mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Mbali na kushirikiana kuhusu Syria, katika sekta ya nishati na ulinzi, uhusiano kati ya Urusi na Iran umeimarika licha ya kutokewa na ushirikiano mkubwa katika nyanja ya kibiashara. Uhusiano huo umeshamiri chini ya utawala wa Rouhani licha ya nchi hizo mbili kuwa na historia tete kati yao kuhusu mafuta, Ukomunisti na maeneo ya mipaka ya nchi.

Rais Rouhani anatafuta kuuimarisha uchumi wa taifa lake kabla ya uchaguzi mkuu mwezi Mei ambapo anatarajiwa kugombea muhula wa pili madarakani. Iran na Urusi zimekuwa zikishirikiana katika kumpa usaidizi mkubwa Rais wa Syria Bashar la Assad ambaye amekuwa akipambana na waasi wanaotaka kumng'oa madarakani.

Nchi hizo mbili zimemsaidia Assad kuyakomboa maeneo mengi kutoka mikononi mwa waasi katika kipindi cha miezi michache iliyopita ikiwemo kulisaidia Jeshi la Syria kulidhibiti eneo la mashariki mwa jimbo la Aleppo, iliokuwa ngome kuu ya waasi.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman