1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Kenya ataka mishahara ya wabunge ipunguzwe

Admin.WagnerD16 Machi 2017

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametoa wito wa kupunguzwa mishahara ya wabunge na maafisa wakuu akisema suala hilo limechangia kuzuka kwa migomo ya wafanyakazi.

https://p.dw.com/p/2ZEee
Kenia Garissa Universität Anschlag Kenias Präsident Uhuru Kenyatta äußert sich zu dem Anschlag
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiwa na makamo wake William RutoPicha: Reuters/Thomas Mukoya

Rais Kenyatta ameyasema hayo alipohutubia kwenye kikao cha pamoja cha Bunge la Taifa na Baraza la Senate katika hotuba yake ya mwisho ya kipindi chake cha kwanza uongozini na kuongeza kuwa viwango vya juu vya mishahara ya wabunge vimesababisha migomo ya wafanyakazi wa sekta nyingine kutaka nyongeza za mishahara. 

Hotuba ya Rais huyo imesheheni majibu ya maswali yanayoulizwa na upinzani kila uchao kuanzia ufisadi, ufujaji wa fedha za umma, kuzorota kwa huduma za afya, elimu na usalama.

Rais Uhuru amejivunia kupungua kwa visa vya mashambulizi ya magaidi nchini, kuongezwa kwa idadi ya maafisa wa usalama na ukuaji wa uchumi ambao amesema umekuwa juu ya kiwango cha makadirio ya taasisi za kimataifa cha asilimia tatu kwa Mwaka.Rais Uhuru ametaja mmoja baada ya mwingine miradi ambayo serikali yake imetimiza katika kipindi cha miaka minne uongozini. Lakini pamoja na yote  kauli iliyoibua hisia ni ile ya kutaka mishahara ya wabunge na maafisa wakuu wa serikali ipunguzwa.

Mishahara ya vigogo ipunguzwe

Bildergalerie Grün in Afrika
Mkenya mweye asili ya Kisomali akipiga kura katika uchaguzi wa 2013Picha: AFP/Getty Images

Amesema viwango vya juu vya mishahara ya wabunbe vimewafanya wafanyakazi katika sekta nyingine kupigania nyongeza za mishahara. Huku zikiwa zimesalia siku 145 uchaguzi mkuu kufanyika Rais Uhuru Kenyatta amechukua fursa ya hotuba hiyo kujipigia upatu ili aweze kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili.

Kinyume na hotuba ya Mwaka uliopita, hotua ya Mwaka huu haikutatizwa na wabunge wa upinzani kama walivyokuwa wameapa kufanya ikiwa Rais hangeomba msamaha wananchi kwa matamshi yake ya matusi katika siku za hivi karibuni. Hata hivyo hilo lilipingwa na mbunge wa Mvita.

Rais Kenyatta amesema kwamba serikali yake imejitolea kuhakikisha uchaguzi wa huru na haki na kuiomba Idara ya Mahakama kutotatiza matayarisho ya uchaguzi ujao. Tayari kesi kadhaa ziko mahakamkani kupinga utaratibu wa tume ya uchaguzi nchini tume ya huru ya uchaguzi nchini humo IEBC.

Rais Uhuru Kenyatta amekumbana na upinzani mkali katika kipindi chake cha kwanza kinachomalizika mwezi wa nane Mwaka huu akilaumiwa kwa kukithiri kwa ufisadi, kuzorota kwa usalama na kupanda kwa gharama ya Maisha. Baada ya kulihutubia taifa kiongozi wa taifa alifungua rasmi jengo la Baraza la Senate na kusema ufunguzi wa ukumbi wa Senete ni ishara ya kuimarika kwa mamlaka ya ugatuzi.

Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Sudi Mnette