1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Somalia aepuka kura ya kutokuwa na imani nae

2 Septemba 2008

-

https://p.dw.com/p/F90q

BAIDOA

Waziri mkuu wa Somalia Nur Hassan Hussein jana aliponusurika katika kura ya kutokuwa na imani nae baada ya kuungwa mkono na wabunge wengi.

Kati ya wabunge wote 200 waliokuweko bungeni ni wabunge sabaa tu waliopiga kura ya kumpinga waziri mkuu huyo.

Wabunge wanaompinga waziri mkuu Nur Hasaan wanamshutumu kwa ufujaji wa fedha za serikali.

Waziri mkuu ameutaja ushindi huo kuwa ushindi kwa watu wa Somalia na wapenda amani.

Hata hivyo wapinzani wa waziri mkuu wanadai shughuli hiyo ya bunge ilitawaliwa na udanganyifu mkubwa kwasababu wabunge walizuiwa kuchangia mada kabla ya kupiga kura.

Serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa imekuwa katika mvutano tangu ilipoundwa mwaka 2004.Wiki iliyopita waziri mkuu na rais walisaini makubaliano ya kumaliza uhasama kati yao ambao ulikuwa ukiihujumu serikali hiyo dhaifu.

Wakati huohuo wanamgambo wa mahakama za kiislamu wametangaza hapo jana kuendelea na mapambano dhidi ya serikali na wanajeshi wa Ethiopia katika mwezi huu wa Ramadhan.

Mzozo wa Somalia na mvutano wa kuwania madaraka uliibuka baada kungolewa madarakani utawala wa dikteta Siad Barre mwaka 1991.