1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Yemen kutoongeza muda wake madarakani

2 Februari 2011

Rais wa Yemen, Ali Abdullah Saleh amesema hatoongeza muda wake madarakani, wala hatomkabidhi madaraka mwanawe wa kiume.

https://p.dw.com/p/108xb
Rais wa Yemen, Ali Abdullah SalehPicha: picture-alliance/ dpa

Wakati sakata la wananchi katika mataifa ya Kiarabu kuwataka viongozi wao waondoke madarakani likiendelea, Rais wa Yemen, Ali Abdullah Saleh, ambaye ni mshirika muhimu wa Marekani, amesema hatoongeza muda wake wa kubakia madarakani, hatua ambayo itamaliza utawala wake wa miongo mitatu, wakati ambapo muhula wake wa sasa utakapolamizika mwaka 2013.

Kutokana na maandamano makubwa yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa Tunisia, Zine El Abidine Ben Ali, na kitisho cha kumuondoa madarakani rais wa Misri, Hosni Mubarak, kinachoendelea kwa sasa, Rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh, leo ameahidi kutoongeza muda wake wa kubakia madarakani, wala hatokabidhi madaraka kwa mtoto wake wa kiume, lakini amewaomba wapinzani kuachana na maandamano.

Akizungumza na bunge, Baraza la Shoura na maafisa wa jeshi, Rais Saleh amesema amechukua hatua hiyo kwa maslahi ya taifa la Yemen, kwa sababu maslahi ya nchi yanakuja kwanza kabla ya maslahi binafsi. Kiongozi huyo wa Yemen ameyatoa matamshi hayo siku moja kabla ya maandamano makubwa yaliyopangwa kufanyika hapo kesho na ambayo yamepewa jina 'Siku ya Ghadhabu', na siku moja pia baada ya Rais Mubarak wa Misri kutangaza kutogombea katika uchaguzi.

Maandamano yaliyopangwa na upinzani

Jemen Demonstration gegen die Regierung in Sanaa
Wananchi wa Yemen, wakiandamana mjini Sanaa, 24 January 2011Picha: picture alliance/dpa

Maandamano hayo yameandaliwa na upande wa upinzani, ikiwa ni katika kufuata kile kilichofanyika nchini Tunisia na kinachoendelea Misri kwa madai ya kutaka mabadiliko ya serikali. Rais Saleh amewatolea wito wapinzani kusitisha mipango hiyo ya kufanya maandamano. Yemen, tayari inaonekana kuwepo ukingoni mwa taifa lililoshindwa, inajaribu kupambana na wapiganaji wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, kupatikana kwa amani kati ya serikali na waasi wa Kishia katika eneo la kaskazini na kukomesha juhudi za kutaka kujitenga katika eneo la Kusini, katika jitihada za kupambana na umasikini ambao umesababisha sehemu ya tatu ya wananchi wa Yemen kukabiliwa na njaa kali.

Tayari Rais Saleh aliahidi kuwepo makubaliano madogo kuhusu mipaka ya madaraka ya rais na kuahidi kuongeza mishahara ya watumishi wa umma na wanajeshi kwa kaisi Dola 47 kwa mwezi. Asilimia 40 ya idadi ya wananchi wa Yemen wanaishi kwa kipato chini ya Dola 2 kwa siku. Rais Saleh pia ametangaza kuahirisha uchaguzi wa wabunge uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Aprili, mpaka mazungumzo na upande wa upinzani kuhusu muungano yatakapokamilika.

Sheria zilizopo sasa

Sheria zilizopo sasa nchini Yemen zinamtaka Rais Saleh kuachia madaraka kama rais wakati muhula wake wa mwisho utakapomalizika mwaka 2013. Lakini baadhi ya wanachama wa chama chake tawala waliwakasirisha wapinzani mwishoni mwa mwaka uliopita kutokana na kuanzisha pendekezo la kuondoa muda huo. Wapinzani nchini Yemen walijaribu kufanya maandamano ya kupinga wazo hilo mwezi Desemba, mwaka uliopita, lakini wananchi wengi hawakujitokeza mitaani. Hata hivyo, wiki iliyopita, upinzani nchini Yemen ulifanikiwa kuwakusanya karibu watu 16,000 katika mitaa mbalimbali wakitaka mabadiliko ya serikali, huku wengine wakimtaka Rais Saleh aondoke madarakani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,DPAE,AFPE)
Mhariri: Miraji Othman