1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Angola José Eduardo Santos afariki dunia

Lilian Mtono
8 Julai 2022

Rais wa zamani wa Angola Jose Eduardo dos Santos amefariki dunia mchana wa leo wakati akipatiwa matibabu Barcelona nchini Uhispania.

https://p.dw.com/p/4DsJ2
Jose Eduardo dos Santos
Picha: Mustafa Yalcin/AA/picture alliance

Jose Eduardo dos Santos amefariki akiwa na umri wa miaka 79 baada ya kuugua kwa muda mrefu, hii ikiwa ni kulingana na tangazo la serikali kupitia ukurasa wake wa Facebook. 

Tangazo hilo limesema dos Santos aliyetawala Angola kwa karibu miaka 40 kuanzia mwaka 1979, alikuwa ni kiongozi wa nchi mwenye hadhi ya kiwango cha kihisoria aliyeipitisha Angola katika nyakati ngumu mno.

Dos Santos amekuwa akiishi Barcelona kwa muda mrefu tangu alipojiuzulu mwaka 2017 na amekuwa akipatiwa matibabu ya matatizo ya kiafya yaliyomsumbua tangu mwaka 2019. Shirika la habari la Ureno la Lusa, liliripoti mwezi uliopita kwamba rais huyo wa zamani alilazwa katia chumba cha uangalizi maalumu hukohuko Barcelona.

Soma Zaidi: Dos santos wa Angola kung'atuka 2018

Afrika Angola Präsident Joao Lourenco in Glasgow
Rais Joao Lorenco wa Angola ametangaza siku tano za maombolezo nchini humo kufuatia kifo cha rais wa zamani dos SantosPicha: Adrian Dennis/AFP/AP/picture alliance

Rais wa sasa wa Angola Joao Lorenco ametangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa kuanzia hii leo, ambapo benderea zitapepea nusu mlingoti na sherehe zote za umma zimesitishwa.

Akiwa Barcelona, binti yake Tchize dos Santos ametoa mwito wa kufanyika uchunguzi kutokana na hofu ya kile anachokitaja kama mchezo mchafu.

Tchize ambaye tayari amefungua kesi dhidi ya mke pamoja na daktari binafsi wa baba yake kwa jaribio la mauaji ameiomba taasisi ya ya tiba ya Teknon kuuhifadhi mwili wa baba yake hadi kutakapofanyika uchunguzi wa kina, kutokana na hofu kwamba huenda ukapelekwa Angola, hii ikiwa ni kulingana na mawakili wake.

Dos Santos mmoja wa marais waliohudumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, aliingia madarakani miaka minne baada ya Angola kupata uhuru kutoka kwa Ureno na baadae kuwa uwanja wa vita vya wakala, katika enzi ya Vita Baridi.

Tizama Video: 

Rais dos Santos kuachia madaraka Angola

Dos Santos, mara kwa mara alijitanabahisha kama rais wa ´bahati mbaya` akipokea kijiti kutoka kwa kiongozi wa kwanza Agostino Neto aliyefariki dunia kwa maradhi ya saratani mwaka 1979.

Utawala wake ulitiwa doa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa karibu miongo mitatu dhidi ya waasi wa UNITA walioungwa mkono na Marekani. Alishinda vita hivyo mwaka 2002.

Nafasi yake ilichukuliwa na Joao Lorenco mwaka 2017, ambaye licha ya kutoka chama kimoja na Santos cha People's Movement for Liberation of Angola, MPLA alianzisha uchunguzi wa madai ya ufisadi wa mabilioni ya dola uliofanyika enzi ya utawala wa Santos.

Mashirika: APE/RTRE