1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyekuwa Rais wa Benin aaga dunia

15 Oktoba 2015

Rais wa zamani wa Benin Mathieu Kerekou aliyejulikana kwa jina la utani 'kinyonga' ameaga dunia. Kerekou aliiongoza Benin kwa miaka 30 baada ya mapinduzi ya serikali na baadaye baada ya chaguzi za kidemokrasia.

https://p.dw.com/p/1Gokz
Picha: AP Photo

Rais huyo wa zamani wa Benin alifariki dunia Jumatano (14.10.2015) akiwa na umri wa miaka 82. Rais wa Benin Thomas Boni Yayi alitangaza kuhusu kifo cha kiongozi huyo na kusema ana majonzi makubwa na kusikitishwa na kifo cha Jenerali Kerekou.

Serikali imetangaza wiki nzima ya maombolezi ya kitaifa kuanzia siku ya Ijummaa huku bendera kote nchini humo zikitarajiwa kupeperushwa nusu mlingoti.Kerekou alijulikana kwa jina lake la maarufu la utani - Kinyonga kutokana na tamko alilotoa wakati alipoingia madarakani mwaka 1972 kuwa anapanga kusonga polepole lakini kwa ufasaha kama kinyonga katika kuiongoza Benin.

Alisifika sana baadaye na kulifanya jina hilo kinyonga kukita mizizi kutokana na uwezo wake wa kubadilisha misimamo yake ya kisiasa kuendana na nyakati.

'Kerekou aliheshimika Benin

Hatimaye, mnamo mwaka 2006 alistaafu akiwa na umri wa miaka 72 kuambatana na katiba ya Benin. Kerekou aliyezaliwa tarehe 2 mwezi Septemba mwaka 1933 ni miongoni mwa wanasiasa wanaoenziwa na kuheshimika sana nchini humo kwa kuweza kuliongoza taifa hilo kama kiongozi wa kijeshi na baadaye kama kiongozi aliyechaguliwa kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.

Rais wa Benin Thomas Bonuses Yayi Boni
Rais wa Benin Thomas Bonuses Yayi BoniPicha: K.Sia/AFP/Getty Images

Baada ya kuhitimu katika vyuo vya kijeshi nchini Mali na Senegal, alijiunga na jeshi la Ufaransa na kupewa mafunzo mjini Paris kabla ya kuwa mlinzi mkuu wa Rais wa kwanza wa Dahomey Hubert Maga.

Kerekou alikuwa kamanda wa jeshi wakati aliponyakua madaraka mwaka 1972 kupitia mapinduzi ya serikali ya Maga kufuatia kipindi cha msukosuko uliotokana na misururu ya mapinduzi tangu Dahomey alipojinyakulia uhuru kutoka kwa wafaransa mwaka 1960 na kubadilisha jina la nchi hiyo kuwa Benin.

Alipendezwa na kile kilichojulikana kuwa 'wimbi la kutaka mageuzi la waliokandamizwa katika ulimwengu wa tatu' na kuanzisha utawala wa falsafa ya Marx na Lenin na kuitangaza Benin kuwa Jamhuri mwaka 1975.

Mwezi Desemba 1989 Kerekou ambaye akipenda sana kuvaa shati lisilo na kola alitangaza kuachana na falsafa ya Marxi kufuatia mzozo mkubwa wa kiuchumi na wimbi la uasi wa umma uliodumu kwa mwaka mmoja.

Mnamo mwaka 1990 Kerekou aliitisha mkutano wa kitaifa wa viongozi wa kisiasa wakiwemo wa upinzani na asasi za kiraia, mkutano wa kwanza wa aina yake barani Afrika ambao ulitoa fursa ya kuanza siasa za vyama vingi barani humo.

Alikiri hadharani mapungufu yake, akaomba radhi na kukubali kuruhusu serikali ya mpito na aliyekuwa afisa wa benki ya dunia Nicephore Soglo kama waziri mkuu.

'Kinyonga' alijibadili rangi kuendana na majira

Soglo alishinda uchaguzi wa rais mwaka 1991 kwa kumshinda Kerekou katika duru ya pili ya uchaguzi. Miaka mitano baadaye Kerekou ambaye alikuwa amestaafu aliibuka tena na kushinda urais akiungwa mkono na wengi wa wanasiasa waliokuwa wakimpinga Soglo.

Hollande in Benin
Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Rais Yayi BoniPicha: Reuters/C.-P. Tossou

Kuchaguliwa tena kwa kiongozi huyo mwaka 2011 kulimfanya kuwa miongoni mwa marais wa Afrika kuwahi kuhudumu kwa muda mrefu zaidi. Kutokana na kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia na bila shati hiyo lake la kola ya Mao, Kerekou alijipatia sifa kama miongoni mwa viongozi wa Afrika walioheshimiwa na viongozi wengine.

Alikuwa mpatanishi wa mizozo kama wa Cote d´Ivoire na kuwa kiongozi wa asasi ya kuimarisha ushirikiano wa karibu kati ya nchi zilizotawaliwa na Ufaransa,zikiwemo Benin, Togo, Niger na Burkina Faso.

Boni Yayi aliyechukua uongozi mwaka 2006 baada ya kustaafu kwa Kerekou anatarajiwa kustaafu mwaka ujao baada ya kuhudumu mihula miwili madarakani ikiwa ni kwa mujibu wa katiba ya Benin.

Mwandishi: Caro Robi/afp,ap

Mhariri: Yusuf Saumu