1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Misri, Mubarak afariki dunia

Lilian Mtono
25 Februari 2020

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak amefariki dunia. Mubarak amefariki Jumanne akiwa na miaka 91, wakati akiwa anapatiwa matibabu kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.

https://p.dw.com/p/3YOCA
Hosni Mubarak Nachruf
Picha: Reuters/A. Abdallah Dalsh

Mubarak aliitawala Misri kwa miaka 30, hadi pale alipoondolewa kufuatia maandamano makubwa ya umma mnamo mwaka 2011.

Alikamatwa mwezi Aprili, 2011 ikiwa ni miezi miwili tangu alipoondolewa mamlakani na baadae kupatiwa matibabu kwenye hospitali za magereza na kijeshi hadi mwaka 2017, wakati alipoachiwa baada ya kusafishwa dhidi ya mashitaka yaliyokuwa yakimkabili ya kuagiza waandamanaji kuuliwa.

Mubarak alihukumiwa kifungo cha maisha jela mnamo mwaka 2012 kwa madai ya kula njama ya mauaji ya waandamanaji 239. Mahakama ya rufaa iliamuru kesi hiyo kusikilizwa upya na hatimaye mashitaka yake yalifutwa na aliachiliwa huru mwaka 2017.

Ägypten Hosni Mubarak
Picha hii ya Hosni Mubarak ilichukuliwa Oktoba 6, 1974, wakati Mubarak alipokuwa akikagua gwaride ya kijeshi, mjini Cairo. Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Koundjakjian

Mwaka 2015 alishtakiwa sambamba na watoto wake wawili wa kiume kwa kuchepusha fedha za umma na kuzitumia kwa kuendeleza mali za kifamilia. Walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.

Wamisri wengi walioishi enzi ya utawala wa Mubarak wanachuhukulia wakati huo kama kipindi cha utawala wa kiimla na ubepari. Kuondolewa kwake mamlakani kulifungua njia kwa Misri kufanya uchaguzi huru na wa kwanza uliomwingiza madarakani rais kutoka vuguvugu la Kiislamu, Mohamed Mursi.

Katika enzi ya uhai wake, Mubarak alisema hakufanya kosa lolote na kwamba historia itamuhukumu yeye kama mzalendo aliyehudumia taifa lake bila ya kuwa mbinafsi.

Mashirika: Reuters