1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Wade kujaribu kupatanisha Cote d´Ivoire

22 Aprili 2010

Jee Juhudi za Rais Campaore Zimekwama ?

https://p.dw.com/p/N36S
Rais wa Senegal Abdoulaye WadePicha: DW

Rais Abdoulaye Wade wa Senegal ameombwa kuwa mpatanishi katika mgogoro wa kisiasa nchini Cote d´Ivoire, jambo ambalo linaashiria kumalizika kwa juhudi za mtangulizi wake Rais Blaise Campaore wa Burkina Faso, ambazo zimeshindwa kuutatua mgogoro huo na kufungua njia ya kufanyika kwa uchaguzi.

Rais Abdoulaye Wade alitarajiwa kuelekea Abidjan leo, huku msemaji wake, Mamadou Mamba Ndiaye akisema kiongozi huyo ameombwa na Rais Laurent Gbagbo wa Cote d´Ivoire azungumze na pande zote husika na kuikwamua hali ya hivi sasa.Msemaji huyo akampamba rais Wade akisema anakwenda huko kama mtu mwenye busara barani Afrika ili kusaidia katika juhudi zote zinazofanyika kuleta suluhisho nchini Cote d´Ivoire.

Nchi hiyo bado imo katika hatua za kuimarisha utengamano baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe 2002-2003 vilivyoigawa sehemu mbili. Uchaguzi wa kwanza baada ya vita uliokuwa ufanyike 2005 haukufanyika kutokana na mzozo uliozuka juu ya suala la kuwapokonya silaha waasi na mabishano juu ya daftari la wapiga kura. Mwezi Februari mwaka huu, rais Gbagbo ambaye kikatiba muda wake umemalizika, aliifukuza kazi tume ya uchaguzi , hatua iliozusha machafuko katika baadhi ya miji. Licha ya kwamba sasa kuna tume mpya , lakini utendaji wake umezorota. Hivi sasa kumeibuka tena mgogoro juu ya suala iwapo waasi wapokonywe silaha kabla au baada ya uchaguzi .

Umoja wa mataifa umesema Viongozi wa pande zote husika wananufaika na hali hii kutokana na visa vya rushwa, na biashara za magendo. Na hizi ni tija ambazo zitatoweka pindi uchaguzi huru na wa haki utafanyika, jambo ambalo limedokezwa pia katika ripoti ya kundi la wataalamu wa Umoja wa mataifa kuhusu Cote dÍvoire iliowasilishwa mbele ya baraza la usalama la Umoja huo, tarehe 12 ya mwezi huu.Mgogoro huo wa kisiasa Cote dÍvoire unazidi kuathiri kiuchumi nchi hiyo , mlimaji mkubwa wa zao la cocoa na kupunguza uwekezaji kutoka n´gambo, katika taifa hilo lililokuwa zamani mfano wa kuigwa katika barani Afrika.Pato la zao hilo mwaka huu linatarajiwa kuanguka zaidi kuliko mwaka jana, ambapo hali ilikuwa mbaya kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliopita.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba kuwasili kwa rais Wade mjini Abidjan leo, kutaashiria mwisho wa juhudi za rais Blaise Campaore wa Burkina Faso. Hadi sasa hakuna taarifa yoyote iliotolewa upande wa Burkina Faso.Rais Wade alishawahi kujihusisha na upatanishi katika migogoro mengine barani Afrika , kama vile Zimbabwe, Madagascar, Mauritania, Niger, Chad na Sudan.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman/Reuters

Mpitiaji:Sekione Kitojo