1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Xi Jinping wa China aondolewa ukomo wa mihula

Daniel Gakuba
11 Machi 2018

Jinping anaweza kuwa rais wa maisha wa China, baada ya bunge la nchi yake kuunga mkono leo Jumapili (11.03.2018) mabadiliko ya katiba yanayoondoa kikomo cha mihula kwa rais ambacho kimekuwepo kwa miaka 30 iliyopita.

https://p.dw.com/p/2u7BE
China Kongress der Kommunistischen Partei Xi Jinping
Picha: Reuters/J. Lee

Bunge la China limeondoa kipengele cha katika ya nchi hiyo kinachoweka ukomo wa mihula kwa rais, na hivyo kumnyooshea njia rais wa sasa Xi Jinping kuweza kuongeza kwa muda usiojulikana. Katika kikao cha bunge hilo cha Jumapili, kura ya kuondoa ukomo wa mihula ya rais imeungwa mkono na wajumbe 2,958 kati ya 2,963 walioshiriki. Wajumbe wawili tu ndio wamepinga mabadiliko hayo ya katiba, na watatu wengine wamejizuia kupiga kura.

Wale waliounga mkono mabadiliko hayo wamesema wamefanya hivyo kwa maslahi ya taifa. ''Nadhani hakuna hata mmoja anayeweza kupinga mabadiliko haya kwa sababu yanatokana na sheria sahihi, tena ya kimaendeleo'', amesema mbunge Chai Wenlong kutoka jimbo la Heilongjiang, muda mfupi kabla ya kura hiyo kupigwa bungeni.

Pan Ping, mbunge mwanamke kutoka jimbo la Guangxi, amesema anayo matumaini kuwa Rais Xi Jinping ataongoza China milele.

Uamuzi wa kushtukiza

Mabadiliko hayo ya katiba ambayo yalitangazwa wiki mbili tu kabla ya kupigiwa kura, yaliwashtua wasomi wengi wa China pamoja na wachambuzi wa siasa za nchi hiyo.

Yalibadilisha kabisa mwelekeo wa siasa za China, ambao kwa miaka 30 iliyopita zimekuwa zikifuata sera ya ''mjumuisho'', kwa lengo la kuepuka maamuzi ya mtu mmoja, ambayo kama ilivyoshuhudiwa wakati wa utawala wa kikomunisti wa Mao Zedong, unaweza kusababisha hatari kubwa.

Chama cha kikomunisti cha China kimekuwa kikibadilisha kiongozi kila baada ya miaka kumi, tangu mwaka 1982 uongozi usio na kikomo ulipoondolewa na rais wa wakati huo, Deng Xiaoping.

Mkakati wa muda mrefu

Lakini, alipoingia madarakani mwaka 2013, Xi Jinping alijilimbikizia madaraka kwa kuwatimua watu ambao wangeweza kuwa wapinzani wake kupitia kampeni kali ya kupambana na ufisadi. Mkakati wake wa kujichimbia madarakani pia ulidhihirika wazi katika mkutano mkuu wa chama cha kikomunisti uliofanyika Oktoba mwaka jana, pale mkutano huo ulipoteuwa kamati kuu ya chama, ambayo haina wajumbe vijana, wala mtu yeyote mwenye sifa ya kuweza kuwa mrithi wa Rais Xi.

Mabadiliko haya ya katiba ya china pia yameunda kamisheni ya taifa ya usimamizi, ambayo wakosoaji wanasema itatumiwa na Rais Xi Jinping kama chombo cha kuwatisha na kuwanyamazisha wapinzani wake.

Mtafiti katika Taasisi ya TS Lombard ya mjini London, Uingereza, Jonathan Fenby, amesema Xi Jinping anataka kutumia mamlaka yake kama Rais, Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti na Mkuu wa Kamisheni ya Kijeshi, kutumia nguvu zake katika siasa za ndani, kutimiza malengo yake kwenye uwanja wa kimataifa.

Wang Qishan aliyewahi kuongoza tume ya kupambana na rusha inayoogopwa sana nchini China, amesema kukipa Chama cha Kikomunisti udhibiti wa mambo yote ya kijamii nchini China, limekuwa lengo la muda mrefu la Xi Jinping.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, afpe

Mhariri: Caro Robi