1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RAMALLAH: Merkel akutana na Abbas

1 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDM

Kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, amekutana na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, mjini Ramallah huko Ukingo wa magharibi wa mto Jordan leo mchana.

Bi Merkel ambaye anafanya ziara ya kwanza katika eneo hilo kama rais wa Umoja wa Ulaya, amesema anaona ufanisi katika juhudi za kuufufua mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

Merkel ameisifu serikali mpya ya umoja wa taifa ya mamlaka ya Palestina lakini akamwambia rais Abbas kwamba serikali hiyo sharti itimize kanuni za pande nne zinazoudhamini mpango wa amani ya Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na kuyalaani machafuko, kuitambua Israel na kukubali kuiheshimu mikataba ya amani iliyofikiwa hapo awali baina ya Israel na Palestina.

Baadaye leo anatarajiwa kukutana na waziri mkuu Ehud Olmert mjini Jerusalem. Hapo awali kansela Merkel alifanya mazungumzo na waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni, mjini Jerusalem mapema leo kabla kulitembelea jumba la makumbusho ya mauaji ya halaiki ya Wayahudi la Yad Vashem.

Bi Merkel pia amepewa shahada ya udaktari ya heshima katika chuo kikuu cha kiebrania mjini Jerusalem hii leo.