1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RAMALLAH:Viongozi wa Israel na Palestine kujadili mpango wa amani

3 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBca

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleeza Rice amekamilisha ziara yake ya siku nne ya Mashariki ya Kati.Kiongozi huyo alimueleza Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kuwa Israel iko tayari kufanya nao majadiliano ya masuala ya msingi kuhusu mpango wa amani wa mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa Bi Rice,Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert anaridhia hatua hiyo na mazungumzo ya kujaribu kuunda taifa la Palestina.Kulingana na afisa mmoja wa ngazi za juu nchini Israel wao wako tayari kufanya majadiliano ila masuala yanayohusu mipaka na hatma ya wakimbizi wa Palestina ni nyeti kujadiliwa kwa sasa.

Shimon Peres ni Rais wa Israel na anaeleza msimamo wao

''Tatizo ni kwamba wanataka kuzungumza ila bila kutumia njia mwafaka.Kwahiyo tunapotaka kujadiliana ili kufikia mwafaka hatujui tumuhusishe nani ndiposa Bi Condoleeza Rice anajitahidi kuwahusisha.Kama wanataka kushiriki basi waje katika meza ya mazungumzo.''

Ziara ya Bi Rice ililenga kufanya maandalizi ya mkutano wa amani wa kimataifa uliopendekezwa kufanyika na Rais George Bush wa Marekani baadaye mwaka huu.