1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Real Madrid washerehekea ubingwa wao

Sekione Kitojo
28 Mei 2018

Real Madrid washangiria taji la tatu mfululizo la Champions League barani Ulaya, Nahodha wa zamani wa Barcelona Carles Puyol asema Barcelona inapaswa  kubadilisha malengo baada  ya Real kunyakua mataji mengi zaidi.

https://p.dw.com/p/2yTEA
Champions League Final - Real Madrid v Liverpool - Ronaldo
Picha: Reuters/H. McKay

Kwa  mwaka  wa  tatu  mfululizo Real Madrid  walisherehekea  taji lao  la  Ulaya  la  Champions League  na  mashabiki  wao  jana Jumapili. Madrid  walirejea  nchini  Uhispania  jana  Jumapili wakitokea  Ukraine  walikolinyakua  kombe  hilo  na  walilitembeza katika  mitaa  ya  jiji  la  Madrid  wakati  maelfu ya  mashabiki wakifurahia  na  kuwashangiria  mabingwa  hao  wapya.

Ukraine Anhänger von Real Madrid und Liverpool Anhänger in Kiew
Shabiki kijana wa Real Madrid akifurahia ubingwa wa tatu mfululizo wa klabu yakePicha: DW

Madrid  walirejea  nchini  Uhispania  baada  ya  kushinda  taji  lao  la 13  la  Ulaya  kwa  ushindi  wa  mabao 3-1 dhidi  ya  FC Liverpool mjini  Kiev  siku  ya  Jumamosi.

Sherehe  hizo  ziliishia  katika  uwanja  wa  Santiago bernabeu uliojaa  mashabiki  lukuki  huku  wachezaji  na  mashabiki  wakipiga kelele  Cristiano Ronaldo abakie  katika  klabu  hiyo.

Hii  ni  kutokana  na  matamshi  ya  mshambuliaji  huyo  wa  Real Madrid mara  baada  ya  ushindi  siku  ya  jumamosi  na  kuashiria katika mahojiano kwamba  anatarajia  kuondoka  kutoka  katika  klabu  hiyo. Alisema "ilikuwa  furaha  kubwa  kuwapo Real Madrid".

Mreno  huyo  alionekana  kuwa  katika hali  nzuri  zaidi  wakati  wa sherehe  hizo  mjini  Madrid  na  kuamsha  matumaini  ya  mashabiki kwamba  hataondoka  kwa  kusema "tuonane mwaka  ujao".

Champions League Final - Real Madrid v Liverpool - Ronaldo
Cristiano Ronaldo mshambuliaji wa Real MadridPicha: Reuters/A. Boyers

Sherehe zilianza kwa  wachezaji  na viongozi  wa  timu  kushiriki katika ibada  katika  kanisa  la  eneo  karibu  na  klabu . Kisha walikutana  na  meya  wa  jiji  na  rais  wa  eneo  hilo  kabla  ya kuzungumza  na  mashabiki  kutoka  katika  dirisha  katika  uwanja wa  Puerta del Sol, moja  kati  ya  maeneo  muhimu  ya  jiji  la Madrid.

Katika  mahojiano  baada  ya  ushindi  mchezaji  wa  kati  wa  Real Madrid  raia  wa  Ujerumani  Tony Kroos  alizungumzia  ushindi  wa timu  yake.

"Nafikiri   katika  kipindi cha  kwanza  tulianza  kuizowea  hali zaidi  na zaidi. Tulichukua  udhibiti  wa  mchezo  na  tulianza  kucheza  vizuri kabla  ya  nusu  ya  kwanza  kwisha. Na  tulianza  kipindi  cha  pili kwa  nguvu  na  kwa  jumla  nahisi tulistahili  kuwa  mabingwa."

UEFA Champions League Achtelfinale Hinspiel Real Madrid vs. SSC Neapel Torjubel Tony Kroos
Mchezaji wa kati ya Real Madrid Tony KroosPicha: Getty Images/AFP/J. Soriano

Vitisho vya  kuuwawa

Kwa  upande  wa  Liverpool  hali  haikuwa  shwari , kwani  baada  ya kuondoka  uwanjani  mshambuliaji  wao  tegemeo Mohamed Salah matumaini  yalififia  na  pia  kupata  pigo  la  pili  kwa  makosa  mawili makubwa  ambayo  hayana  maelezo  sahihi  kutoka  kwa  mlinda mlango  wa  timu  hiyo Loris Karius. Shabiki  mmoja  wa  Liverpool Rob  Middleton  ambaye  alisafiri  kutoka  New Zealand  kuja kushuhudia  pambano  hilo  mjini  Kiev , hakuweza  kuzuwia  shutuma zake kwa  Loris Karius.

Polisi  nchini  Uingereza  itafanya  uchunguzi  wa  vitisho  vya  kuuwa vilivyotolewa  dhidi  ya  mlinda  mlango  huyo  wa  Liverpool  Loris Karius  baada  ya  mchezo  huo  wa  Champions League. Karius alishambuliwa  katika  mitandao ya  kijamii  baada  ya  makosa yake mawili kuisaidia  Real Madrid  kushinda  ubingwa  wa  Champions League, ambapo wengi  walioandika  walimuombea  kifo Mjerumani huyo  na  famialia  yake.

Champions League Final - Real Madrid v Liverpool - Niederlage für Liverpool
Loris Karius mlinda mlango wa FC LiverpoolPicha: Imago/MIS/B. Feil

"Nina  maana ,ni  bahati  mbaya  kile  alichofanya  jioni  ya  leo  lakini nafikiri  utakuwa  mchezo  wake  wa  mwisho kwa  Liverpool leo. Lakini  huu  ni  mchezo  ambao haumsubiri  mtu na  nafikiri  hilo linaweza  kutokea mwanzoni  mwa  msimu ujao. sifikiri  kama atacheza tena."

Nae nahodha  wa  zamani  wa  Barcelona Carles Puyol amekasirika , baada  ya  real Madrid  kushinda  Champions League  kwa  mara  ya 13  na  kusema  klabu  hiyo  ya  Catalonia  inapaswa  kubadilisha malengo  yake msimu  ujao. "Naamini  tuna  kikosi  kizuri  kuliko Madrid, lakini  wameshinda  mara nne  katika  misimu  mitano  ya Champions League,"  Puyol  aliliambia  gazeti  la  mjini  Barcelona la  Vanguardia leo Jumatatu.

"Nafikiri  suluhisho  litakuja  baada  ya  kuweka malengo yetu sawa. Tunapoteza  fursa , nimekasirika  kuhusu  hilo kama shabiki  wa Barca. "Kushinda mataji  matatu katika  msimu  ni  ngumu  mno  kama takwimu  zinavyoonesha, kwa  hiyo  nafikiri jambo zuri  la kufanya itakuwa  kuachana  na  kombe  la  Mfalme. Puyol ameongeza kwamba  vikombe  vingine  wapewe nafasi  vijana  kuonesha  uwezo wao na  wachezaji  wa  kikosi  cha  kwanza  washughulike na  ligi  na Champions League.

Carles Puyol
Carles Puyol nahodha wa zamani wa BarcelonaPicha: dapd

Kocha  wa  Ujerumani Joachim Loew  karibu  tayari  amekwisha kamilisha  kikosi  chake  cha  awali  kwa  ajili  ya  mazowezi  leo Jumatatu  katika  kituo  cha mazowezi  ya  timu  hiyo cha  Eppan nchini  Italia.

Mchezaji  wa  kati  ya  Real Madrid  Tony Kroos  antarajiwa  kujiunga na  kikosi  hicho cha  mabingwa  watetezi  wiki  hii , wakati  mlinzi wa  Bayern Jerome Boateng  anaendelea  kupata  nafuu  kutokana na  maumivu  ya  paja.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / rtre / dpae

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman