1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Repoti yastiri ukiukaji wa haki za binaadamu wa vita vya ugaidi.

Mohamed Dahman9 Machi 2007

Repoti ya kila mwaka ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani juu ya haki za binaadamu iliotolewa wiki hii inataja maafa ya kibinaadamu nchini Sudan na kushindwa kwa Rais Pervez Musharraf wa Pakistan kuboresha rekodi ya haki za bnbinaadamu nchini humo kuwa ni baadhi ya nyendo za kutiliwa mashaka katika kuheshimkwa kwa haki za binaadamu za kimataifa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

https://p.dw.com/p/CB5N
Marekani inashutumiwa kwa kukiuka haki za wafungwa inaowashikilia katika magereza ya siri likiwemo Guantanamo kama inavyonekana pichani.
Marekani inashutumiwa kwa kukiuka haki za wafungwa inaowashikilia katika magereza ya siri likiwemo Guantanamo kama inavyonekana pichani.Picha: AP

Repoti hiyo inaanza kwa kukiri kwamba hatua zilizochukuliwa na Marekani katika Vita vya Ugaidi Duniani zimeleta madhara kwa sifa ya Marekani kama mtetezi wa Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binaadamu kwa Dunia.

Repoti hiyo ambayo mara ya kwanza ilipewa baraka zake na bunge la Marekani hapo mwaka 1976 inahusu hali ya haki za binaadamu kwa karibu nchi 200 kwa mwaka 2006 na ina kurasa zaidi ya 3,000.

Kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma repoti ya mwaka huu haigusii hali ya haki za binaadamu nchini Marekani au katika vituo vinavyodhibitiwa na Marekani kama vile kituo cha mahabusu cha kambi ya wanamaji wa Marekani huko Guantanamo Cuba na nchini Afghanistan ambapo serikali ya Marekani imekuwa ikiwashikilia watuhumiwa katika vita vyake vya ugaidi katika hali baadhi ya wachunguzi wa haki za binaadamu wakiwemo wajumbe maalum wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binaadamu waliyosema kwamba ni sawa na kuwa katika mateso.

Nchi zilizotajwa kupiga hatua kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni pamoja na Liberia,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,Haiti, Ukraine na Kyrgystan.

Hata hivyo uchunguzi mpya juu ya Liberia wa ActionAid shirika la maendeleo lka kimataifa lenye makao yake nchini Afrika Kusini limekuja na hitimisho tafauti wiki hii kwa kusema kwamba vitendo vya matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake na ubakaji vinaendelea bila ya kudhibitiwa nchini humo.

Pakistan,Misri,Kazakhstan,Urusi,Venezuela,Fiji na Thailand zimetajwa kuwa ni mfano wa nchi ambapo serikali zimekuwa zikijilimbikizia madaraka na kupunguwa kuwepo kwa uwazi na utawala wa kidemokrasia.

Wakati Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu la Amnesty International likikaribisha sisitizo la kuwajibika la repoti hiyo linasema hadi hapo Marekani itakapobadili sera zake zenyewe za kuwashikilia mahabusu kwa muda usiojulikana katika magereza ya siri na bila ya kuwapa haki za msingi za binaadamu haiwezi kuaminiwa kuwa kiongozi wa haki za binaadamu duniani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo la Kimataifa tawi la Marekani Larry Cox amesema katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kwamba ukiukaji wa haki za binaadamu haupaswi kufichwa nyuma ya unafiki wa kauli mbiu ya usalama wa taifa.

Nchi zilizotajwa kurudi nyuma sana katika haki za binadamu na serikali za demokrasia ni pamoja na Iraq,Afghanistan, Lebabon na Timor ya Mashariki na nchi zilizowekwa katika kundi la serikali zilizobobea katika uvunjaji wa haki za binaadamu ni Korea Kaskazini,Burma,Iran,Zimbabwe,Cuba,China,Belarus na Eritrea.

Repoti hiyo ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani juu ya haki za binaadamu pia inazungumzia wale wanaona kuwa wanatishiwa na mabadiliko ya kisiasa na kijamii ambao wanaweka vikwazo dhidi ya makundi ya kiraia na waandishi wa habari na ukatili dhidi ya waandishi mambo ambayo imesema yanafanyika nchini Urusi,Belarus,Kazakhstan,Turkmenistan,Uzbekistan,Syria, Iran,Burundi,Rwanda,Venezuela,China na Vietnam.

Na hatimae repoti hiyo inatowa wito wa kuwekwa nadhari kwa mauaji ya umma na kupotezewa makaazi katika jimbo la Dafur nchini Sudan pamoja na kuongezeka kwa umwagaji damu katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2006 kulikopelekea kuondoka kwa mashirika kadhaa yasio ya kiserikali na yale ya kibinaadamu.