1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Republican: Chama kilicho njiani kujisambaratisha

Admin.WagnerD5 Agosti 2016

Warepublican wameshindwa kutafuta njia ya kuzuwia matamshi makali yanayotolewa na mgombea wao wa urais Donald Trump. Ines Pohl mjini Washington, anasema chama hicho ndio kilichojenga mazingira kinamojikuta hivi sasa.

https://p.dw.com/p/1JcJa
USA Republican National Convention in Cleveland Donald Trump Rede
Picha: Reuters/M. Segar

Kadiri mambo yanavyozidi kukanganya, ndivyo mtu anapozidi kutamani kurudisha wakati nyuma. Kwa mfano, mwanzoni mwa mwaka huu. Kwa sababu wakati huo, ilikuwa bado wazi kabisaa kuhusu nani angekuwa mteule wa ugombea wa nafasi ya urais kwa vyama vikuu viwili. Sehemu kubwa ya dunia ilidhani Jeb Bush wa Republican na Hillary Clinton wa Democratic wangechuana kuingia ikulu ya White House.

Ni tukio la nadra la kila mwana na lisilo la kidemokrasia lakini ilionekana kuwa wanachama wa himaya hizi mbili za kisiasa - Bush na Clinton - walikuwa na nafasi ya kupata wadhifa huo muhimu zaidi wa kisiasa. Lakini zikiwa zimesalia chini ya siku 100 kuelekea siku ya uchaguzi, kila kitu kimebadilika.

Kwa hakika Clinton ndiye mgombea wa Wademokrat. Lakini alilaazimika kupambana kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyotarajiwa, na alipata tu ushindi wake dhidi ya Bernie Sanders kwa sababu uongozi wa chama cha Democratic ulicheza rafu, ukakabiliana mapema na mpinzani wake na kumpiga vita kwa kila njia.

Mkakati huo ulibainika wazi katika mkesha wa mkutano mkuu wa chama, na kumlaazimu kiongozi wa chama Debbie Wasserman Schultz kujiuzulu. Sakata hilo pia lilithibitisha kwa baadhi namna chama cha Democratic kilivyokumbwa na rushwa.

Kadi mbili za turufu za Trump

Warepublican hawakuchukuwa tahadhari sana na hawakuweza kupata mkakati wa kumuondoa Donald Trump. Badala yake, kinyume na matarajio yote, Jeb Bush na majina mengine maarufu katika chama walilaazimika kumuachia uwanja Donald Trump. Trump alishinda kwa kadi mbili za turufu, ambazo hayuko tayari kuziachia hadi siku ya uchaguzi Novemba 8.

Pohl Ines Kommentarbild App
Mwandishi wa DW Washington Ines Pohl

Kadi yake imara zaidi ni hadhi yake ya kuwa mtu wa nje ya mfumo. Anaweza kutumia hoja kuonyesha kuwa hahusiki na mfumo wa kisiasa wa sasa. Ingawa mfanyabiashara huyo ana mahusiano ya karibu na watu walioko ndani ya mfumo huo, hajajiingiza katika matatizo ya vyama vyote. Matokeo yake ni kwamba anaaminiwa na wananchi wengi wanaoamini kuwa mfumo wa sasa ni klabu makhsusi ya wanasiasa wanaotoka nafasi moja kwenda nyengine. Wanaangaliwa kama watu wanaotazama kwanza maslahi yao kabla ya yote, na kutowajali raia waliowengi.

Kadi nyeingine ya Trump ni ahadi yake ya kuifanya Marekani kuwa taifa kubwa tena. Kuhusu hili, hoja zake nyingi ni za kibaguzi, chuki na dhidi ya maslahi ya wanawake. Lakini kuna kitu zaidi ya hapo: Matarajio kwamba kukiwa na Rais Trump kutakuwa na sera za matokeo kuliko katika miaka iliyopita, ambazo zimekuwa sera za kuzuwia. Kwa hili, Warepublican wanapaswa kujilaumu wenyewe. Kwa sababu zilikuwa hila za ucheleweshaji za chama hicho dhidi ya chama cha Democratic bungeni zilizouzuwia utawala wa rais Obama kufanya kazi yake.

Mfumo wa kisiasa uliyorubiniwa

Ni kwenye mambo hayo mawili ambapo Trump amejengea kampeni zake. Wakati viongozi wa chama kama Paul Ryan wanapomshambulia na kukataa kumuunga mkono, au wakati Warepublican maarufu kama vile Meg Whiteman wanapobadili kambi na kuhamia kwa Clinton, huo kwa wafuasi wa Trump ni ushahidi zaidi wa mahusiano baina ya wanasiasa na namna mfumo mzima ulivyojaa rushwa.

Donald Trump anawezekana tu kwa sababu kuna chembe ya ukweli katika matamshi yake. Hata kama mwenyewe ni mnufaikaji hatari wa ujumbe wake, bado inasalia kuwa kweli. Uongozi wa kisiasa wa taifa hilo, ambalo mara nyingi linatajwa kuwa demokrasia kubwa zaidi duniani, umepoteza mawasiliano na raia. Wapigakura wanahisi hofu na mahitaji yao havionekani wala kusikika.

Kushindwa kwa vyama hivyo viwili vikubwa kutafuta suluhu za kisiasa, na kupoteza kwao imani ya wananchi katika miaka ya hivi karibuni kupitia kueleza uongo ndani ya mifumo ya rushwa kumefungua milango kwa watafuta umaarufu kama Trump.

Uongozi bila majibu

Hadi sasa uongozi wa Republican haujapata jibu kuhusu mashambulizi ya Trump, ambayo anazidi kuyaelekeza kwa chama hicho chenyewe. Matusi yana uwezekano wa kuimarisha nafasi ya Trump. Hakuna uwezekano kwa chama kuchagua mgombea mbadala. Kwa mujibu wa kanuni za chama, ni Trump pekee anaeweza kusafisha njia ya kuteuliwa mgombea mwingine wa Urais wa Republican, ikiwa atajiondoa. Hilo kwa sasa ni gumu kufikirikika.

Trump ameweka wazi kwamba ikiwa atashindwa, ataulamu mfumo wa rushwa, ambao laazima utakihusisha chama cha Republican.

Mwandishi: Ines Pohl/DW Washington/http://bit.ly/2aNzVjW

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Saumu Yusuf