1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice Mashariki ya kati

Hamidou, Oumilkher5 Machi 2008

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani ahimiza mazungumzo ya amani yaendelezwe haraka

https://p.dw.com/p/DII9
Waziri wa nje wa Marekani Condoleezza Rice na mopatanishi wa Palastina Saeb ErakatPicha: AP


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice anaendelea kuwashinikiza waisrael na wapalastina warejee haraka katika meza ya mazungumzo ya amani, yaliyodhoofishwa na mashambulio ya Israel katika Gaza.


Hii leo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice amepangiwa kuzungumza na wakuu wa ujumbe wa Palastina katika mazungumzo ya amani,Ahmad Qorei na Saeb Erakat mjini Jerusalem kabla ya karamu ya chakula cha mchana pamoja na waziri mwenzake wa Israel Tzipi Livni,siku moja baada ya mazungumzo yake pamoja na rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.


Katika wakati ambapo bibi Rice anaendelea na juhudi zake za amani,matumizi ya nguvu yamekua yakiendelea Gaza.Mtoto mchanga wa mwezi mmoja,msichana mdogo Amira Abou Asr na mwanaharakati wa Jihad Youssef Al-Smeiri wameuliwa jana usiku jeshi la Israel lilipovamia kusini mwa ardhi ya wapalastina.Watu wengine kumi wamejeruhiwa katika mapigano hayo kati ya wanajeshi wa Israel na wanaharakati wa kipalastina.


Jana waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice alikwenda Ramallah,kwa ziara ya saa kadhaa,akitokea Cairo na kutoa mwito mazungumzo ya amani yaanze haraka iwerzekanavyo ,baada ya rais wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas kuamua kusitisha mazungumzo hayo jumapili iliyopita akilalamika dhidi ya hujuma za kijeshi za Israel ziliziogharimu maisha ya wapalastina wasiooungua 125 huko Gaza tangu February 27 iliyopita.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani bibi Condoleezza Rice amesema:


"Nimesema pia kwamba ni muhimu kupita kiasi kutilia maanani kitakachofuatia baadae,kwamba kuna haja ya kuwa na washirika ambao watu watalazimika kufanya kazi pamoja nao na kwamba watu wasiokua na hatia ambao kwa bahati mbaya wanajikuta katika maeneo yanayodhibitiwa na Hamas,wasiangulie mhanga kwa kujeruhiwa na kuuliwa."


Licha ya mwito huo rais wa utawala wa ndani wa Palastina mahmoud Abbas amekwepa kutoa ahadi yoyote ile ya kurejea katika meza ya mazungumzo,akishadidia juu ya umuhimu wa kusitishwa mapigano huko Gaza na katika ukingo wa magharibi ili kama alivyosema tunanukuu: "mwaka 2008 uwe mwaka wa kukamilishwa lengo lao la kupatikana amani."Mwisho wa kumnukuu.


Vizuwizi lazma viondolewe na vivukio vifunguliwe upya ili wapalastina waweze kua na maisha ya kawaida na kutojiachia kushawishiwa na Hamas" ameongeza kusema rais Mahmoud Abbas.


Utawala wa Marekani hautarajii kuona mazungumzo ya amani yanaanza mara moja,lakini angalao katika kipindi cha siku chache zijazo.


Mjini Washington rais George W. Bush amesema "ana matumaini mema" sawa na alivyokua kabla ya mkutano wa Annapolis ,kuhusu nafasi ya kufikiwa amani kati ya Israel na Wapalastina kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2008.


Rais Bush amesema hayo baada ya mkutano pamoja na mfalme Abdallah wa pili wa Jordan mjini Washington.

Wakati huo huo Marekani inapanga kuwapatia wapalastina misaada ya kiutu yenye thamani ya dala milioni 148.


Kabla ya kukutana na wapatanishi wa Israel na Palastina hii leo,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice alipangiwa kuzungumza na Dov Weisglass aliyewahi kua mpatanishi wakati wa utawala wa Ariel Sharon.Atazungumza pia na waziri wa ulinzi Ehud Barak aliyonya opereshini ya kijeshi ya Israel itaendelea Gaza.