1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti juu hali ya usalama wa chakula.

Halima Nyanza19 Agosti 2010

Afghanistan na nchi nyingine tisa kutoka barani Afrika zinaongoza katika orodha ya kutokuwa na usalama wa chakula.

https://p.dw.com/p/OrJD
Mshirika ya misaada ya kimataifa yakipeleka misaada katika maeneo ya Afghanistan. nchi ambayo inaongoza kwa kutokuwa na usalama wa chakula, kulingana na ripoti iliyotolewa leo.Picha: AP

Ripoti ya hali ya usalama wa chakula kwa mwaka 2010 iliyotolewa leo imeeleza pia kwamba nchi kutoka Amerika ya kaskazini na Ulaya magharibi, hususan nchi za Scandinavia zina uhakika wa usambazaji wa chakula.

Ripoti hiyo juu ya usalama wa chakula kwa mwaka 2010, ambayo imeandaliwa na asasi ya utafiti ya Uingereza ya Maplecroft, kwa kuzingatia vyanzo 12 vilivyokusanywa kwa ushirikiano na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa -WFP.

Vigezo vilivyozingatiwa ni pamoja na uzalishaji wa nafaka, pato la ndani la nchi, hatari inayoikabili nchi husika kuhusiana na majanga mbalimbali yanayotokana na hali ya hewa kama vile ukame na mafuriko, ubora wa kilimo na miundo mbinu, mizozo na nguvu ya serikali ya nchi husika.

Orodha hiyo ya nchi 10, zilizo katika hali mbaya zaidi ambayo inaongozwa na Afghanistan, inataja pia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Eritrea, Sudan, Ethiopia, Angola, Liberia, Chad na Zimbabwe.

Nchi hizo za Afrika zimekuwa zikikabiliwa na umasikini na pia tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa.

Mtafiti wa masuala ya mazingira wa asasi hiyo ya Maplecroft  Fiona Place amesema kati ya nchi 50, ambazo ziko katika hatari, zaidi 36 ziko kusini mwa jangwa la Sahara

Nchi nyingine zilizotajwa ni pamoja na Bangladesh, Pakistan, India na Philippines.

Naye Mkuu wa asasi hiyo ya utafiti ya Uingereza ya Maplecroft, Alyson Warhurst amesema Pakistan na nchi zilizokusini mwa jangwa la Sahara ambazo zinategemea chakula kutoka nje zitaendelea kuathirika zaidi.

Pakistan ambayo inashika nafasi ya 30 katika orodha hiyo, kwa sasa iko katika jitihada za kukabiliana na  mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo, ambayo yameshaua watu 1,600 na kuathiri vibaya sekta ya kilimo.

Mataifa yaliyotajwa kuwa na usalama mzuri wa chakula ni Finland, Sweden, Norway pamoja na Marekani.

Aidha asasi hiyo ya utafiti ya Maplecroft imesema mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha kupanda kwa bei ya ngano. na kutolea mfano Urusi ambayo kuanzia Agusti 15 mwaka huu ilipiga marufuku usafirishaji wa nafaka nje ya nchi hiyo.

Nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na janga la moto wa msituni, ambao tayari umeshateketeza hekari kadhaa na kuathiri sekta ya kilimo.

Asasi hiyo imesema hatua ya Urusi kupiga marufuku usafirishaji wa nafaka, utaifanya China kusambaza zaidi chakula katika soko la dunia. na kuongeza kusema kuwa matukio yanayotokana na hali mbaya ya hewa ambayo yameikumba Pakistan na Urusi, matokeo yake yatasababisha hatari zaidi ya hali ya usalama wa chakula kwa mwaka ujao katika nchi hizo.

Katika kipindi cha mwaka uliopita ripoti ya hali ya chakula iliyotolewa na asasi hiyo, Angola iliongoza ikifuatiwa na Haiti, Msumbiji, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Eritrea, Zambia, Yemen, Zimbabwe na Rwanda.

Mwandishi: Halima nyanza( Reuters afp)

Mhariri: Abdul-Rahman