1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya FAO kuhusu njaa 2010

14 Septemba 2010

Idadi yapungua akilinganishwa na 209

https://p.dw.com/p/PBsX
Ukame huchangia matatizo ya njaa na ukosefu wa chakula boraPicha: Simone Schlindwein

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa mataifa FAO, limesema idadi ya watu wanaokabiliwa na janga kubwa la njaa duniani imepungua kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15, kwa sababu ya kuboreka kwa hali za kiuchumi na bei za chini za chakula. Ripoti ya shirika hilo inasema kiasi ya watu 925 milioni wana ukosefu wa chakula bora mwaka huu wa 2010, kutoka bilioni 1.02 mwaka jana ambapo ilikuwa ni idadi kubwa kabisa katika kipindi cha miongo minne.

Licha ya kupungua kwa tatizo hilo sugu la ukosefu wa chakula bora, kama ilivyoripotiwa na Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa mataifa, machafuko yaliotokana na kupinga hatua za kupandishwa bei za vyakula nchini Msumbiji mapema mwezi huu, maandamano ya upinzani huko Misri na ongezeko la bei za nafaka kutokana na ukame nchini Urusi, ni mambo yaliolirudisha tena suala la njaa na usalama wa chakula katika ajenda ya dunia.

Shirika la FAO linasema wengi miongoni mwa watu wenye njaa duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea, ambao ni 16 asili mia ya idadi ya 2010 ya wakaazi duniani,

Wakati hali imeboreka kutoka asili mia 18 mwaka jana 2009, FAO linaonya kwamba bado idadi iko nyuma sana ya lile lengo la Umoja wa mataifa, la kupunguza idadi ya watu wenye nafasi duni za kupata chakula katika nchi zinazoendelea kutoka 20 asili mia mwaka 1990-92 hadi asili mia 10 katika mwaka 2015.

Ripoti yake inasema tatizo kubwa bado lingalipo kwa sababu karibu watu bilioni moja bado wanakabiliwa na njaa hata baada ya kumalizika kwa msukosuko wa hivi karibuni wa chakula na fedha.

Lakini wakati mkutano huo ukisubiriwa, wakala mmoja wa misaada umesema athari za njaa zinaweza kuzigharimu nchi zinazoendelea dola bilioni 450 kwa mwaka. Katika ripoti yake mpya wakala huo ActionAid umeonya kuhusu gharama hizo za juu ambazo ni sawa na euro 350 bilioni, na kuzingatia juu ya juhudi za kupunguza tatizo la njaa katika nchi 28 zinazoendelea.

Ripoti hiyo imegunduwa kwamba nyingi kati ya nchi hizo zinashindwa katika juhudi zao za kupunguza njaa hadi nusu ifikapo 2015, lengo kuu la maendeleo. Kwa mujibu wa uchambuzi wake,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi,Sierra Leone, Pakistan na Lesotho ndizo zenye matatizo makubwa zaidi ya kupunguza viwango vya njaa.

Viongozi wa dunia wanatarajiwa kutangaza wakati wa mkutano wao wa kilele wiki ijayo kwamba malengo kadhaa yanayokusudiwa katika kupunguza umasikini na njaa kote duniani ifikapo 2015 yanaweza kufikiwa, ikiwa ni kwa mujibu wa rasimu ya hati itakayowasilishwa mkutanoni.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman /reuters/afp

Mpitiaji:Josephat Charo