1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Goldston-Umoja wa Mataifa

15 Oktoba 2009

Israel yadai ni ya upande mmoja-Palestina yadai itekelezwe.

https://p.dw.com/p/K6dd
Hakimu Richard Goldstone.Picha: AP

Huko Umoja wa Mataifa, Waisraeli na Wapalestina, jana walishinikizwa na mataifa mbali mbali wakitakiwa kujibu ipasavyo ripoti ya Umoja wa Mataifa, inayodai kufanyika uchunguzi wenye kuaminika nchini mwao kuhusu visa vya uhalifu wa vita vinavyodaiwa kutendeka wakati wa vita vya Gaza mwaka jana.

Israel kwa upande wake inadai ikiwa itaendelea kutuhumiwa kutenda uhalifu huko Gaza,haitaweza kuwaridhia wapalestina mambo kadhaa yanayoweza mwishoe kuleta mapatano ya amani.Chama cha Hamas kinacho tawala Gaza, kinahisi kimefaidika na kuchapishwa kwa ripoti hiyo ya hakimu wa Afrika kusini ,Richard Goldstone.

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon, alihimiza kufanywa uchunguzi huo wakati wa mjadala wa jana juu ya Mashariki ya Kati ambao wapalestina na wafuasi wao , waliutumia kuanika hadharani madhambi yaliomo kwenye ripoti hiyo jinsi Israel ilivyoendesha vita vyake vya wiki 3 mwambao wa Gaza.

Kiasi cha wapalestina 1.400 na waisraeli 13 waliuwawa katika vita vile vilivyoripuka pale Israel, ilipoanzisha hujuma kali ya kijeshi huko Gaza hapo Desemba 27,mwaka uliopita ili kujibisha hujuma za makombora yaliofyatuliwa na wanamgambo wa kipalestina.

Ripoti ya Tume ya UM ilioongozwa na jaji maarufu wa Afrika kusini,Richard Goldstone,imezituhumu pande zote mbili-Israel na wanamgambo wa Palestina kutenda uhalifu wa vita na hata pia uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati wa vita hivyo vya muda wa wiki 3.

Uingereza,Ufaransa na Marekani ,ziliungamkono mwito wa katibu Mkuu Ban Ki-moon.Mjumbe wa Uingereza katika UM, John Sawers, aliliambia Baraza la Usalama na ninanukulu,

"Tunaitaka serikali ya Israel kufanya uchunguzi kikamilifu,wenye kuaminika na usiopendelea juu ya mashtaka yaliotolewa katika ripoti ya Bw.Goldstone."

Makamo wa mjumbe wa Marekani katika UM Alejandro Wolff, ambae nchi yake ni mshirika wa chanda na pete wa Israel, alikariri tu wasi wasi mkubwa wa nchi yake juu ya ripoti ya Bw.Goldstone na kudai kwamba, haina wezani na inailaumu zaidi Israel....Alisema pia kwamba, Marekani, hatahivyo, inaitia maanani ripoti hiyo.

Nae mjumbe wa Israel katika Umoja wa Mataifa, bibi Gabriela Shalev, alirudia msimamo wa nchi yake kuiüinga moja kwa moja ripoti ya Bw.Goldstone.Hii inafuatia hoja iliotoa Israel hapo kabla katika jaribio lake la kuzima mjadala juu ya ripoti hiyo kuwa, kuidhinisha ripoti ya Goldstone, ni kuzika matumaini yoyote ya kuanzisha upya mazungumzo ya amani ya mashariki ya Kati.

Akilihutubia Baraza hilo la Usalama,waziri wa nje wa Palestina,Riyad al-Malki, alishikilia kwamba, mapendekezo yaliomo katika ripoti ya Bw.Goldstone, yatekelezwe barabara.Akalitaka Baraza la Usalama,Baraza Kuu la UM na Mahkama ya Kimataifa inayohusika na uhalifu kuchukua hatua.

Mwandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: M.Abdul-Rahman