1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti: COVID -19 yasababisha vifo kwa wafungwa nchini Misri

Zainab Aziz Mhariri:Josephat Charo
20 Julai 2020

Shirika la haki za binadamu la "Human Rights Watch", limesema katika ripoti yake kwamba baadhi ya magereza ya nchini Misri na kwenye vituo vya polisi ni maeneo ambayo yanakabiliwa na milipuko ya Covid-19.

https://p.dw.com/p/3fbVX
Human Rights Watch Logo Symbolbild
Picha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Katika ripoti yake hiyo ya tarehe 20.07.2020, shirika la Human Rights Watch limesema ushahidi ulio mikononi mwake ambao ni barua zilizopenyezwa kutoka kwenye magereza mawili, pamoja na ripoti za kuaminika kutoka kwa makundi ya kiraia na kwenye vyombo vya habari, jumla ya wafungwa 14 waliokuwemo gerezani na mahabusu katika vituo 10 vya jela za mwanzo wamekufa kutokana ugonjwa wa Covid-19, mnamo tarehe 15 mwezi huu.

Ripoti hiyo imesema magereza kadhaa nchini Misri yanatoa huduma duni za matibabu na wala hayana vifaa vya kufanyia uchunguzi wa virusi vya corona. Licha ya mamlaka kuwaachia huru wafungwa wapatao13,000 tangu mwishoni mwa mwezi Februari, idadi hiyo haijasaidia kupunguza msongamano uliopo magerezani na pia kwenye vituo vya kuwazuia mahabusu wanaosubiri kesi zao.

Shirika hilo la haki za binadamu "Human Rights Watch" limesema maafisa wake waliwahoji wafungwa katika magereza matatu, waliwahoji ndugu 10 wa wafungwa hao, na pia waliwahoji marafiki wa wafungwa 11 walio katika magereza mengine sita na kwenye kituo kimoja cha polisi.

Gereza la Tora mjini Cairo
Gereza la Tora mjini CairoPicha: Reuters/A.A. Dalsh

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu pia limezipitia upya taarifa rasmi, ripoti za vyombo vya habari, za shirika la haki za binadamu na pia ripoti za Shirika la Afya Ulimwenguni WHO pamoja na mwongozo wa Wizara ya Afya ya Misri kuhusu Covid-19 na kisha kuiuliza maswali Misri. Hata hivyo Wizara ya Mambo ya ndani, idara ya Habari ya Misri, na ubalozi wa nchi hiyo mjini Washington, DC hazikujibu maswali hayo ya Human Rights Watch yaliyotumwa mnamo tarehe 3 na tarehe 15 mwezi huu.

Human Rights Watch imesema kutokana na ushahidi uliotolewa na taarifa zilizopo inaonyesha wazi kuwa msongamano magerezani ndio sababu inayoleta ugumu wa kulitekeleza zoezi la kuwaweka watu mbali na wenzao ili kukidhi kigezo cha kuweka nafasi kati ya mtu na mtu kwa ajili ya kunguza uwezekano wa kuambukizana.

Kamati huru ya haki za binadamu ya mjini Geneva, Uswisi imesema imeorodhoshesha zaidi ya watu190 wanaohofiwa kuwa wanaugua Covid-19 katika magereza 12 na kwenye vituo 29 vya polisi, wakiwemo wafungwa zaidi ya 160. Wafanyakazi wapatao 30 wa Wizara ya Mambo ya Ndani na askari ni miongoni mwa watu walioambukizwa.

Joe Stork, naibu mkurugenzi wa Shirika la Human Rights Watch kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini amesema mamlaka ya Misri inapaswa kuchukua hatua za haraka ili kumpa kila mtu aliye kizuizini huduma za kutosha za matibabu, amesema ni muhimu kwa Misri kuzingatia hatua za kuwachia wafungwa kutoka gerezanikama njia mojawapo ya kuendeleza mapambano dhidi  kuenea kwa virusi vya corona.

Chanzo: Human Rights Watch