1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mwaka 2006ya taasisi ya IPI juu ya uandishi habari

27 Aprili 2007

Tathmini ya mwaka juu ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari inaeleza kwamba mwaka 2006 ulikuwa mwaka mbaya kwa waandishi wa habari ambapo kiasi wanahabari 100 waliuwawa.

https://p.dw.com/p/CB4Q

Tathmini hiyo imetolewa na taasisi ya kimataifa ya habari ya mjini Vienna Austria.

Leo tunaangalia Uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania.

Nchini Tanzania kuna sheria kadhaa ambazo zinazuia uwezo wa vyombo vya habari kuripoti kwa njia huru.

Sheria ya uandikishaji magazeti inaruhusu serikali kuandeikisha na kuyafungia magazeti kwa ajili ya maslahi ya amani na maadili na upande mwingine sheria inayosimamia matangazo ya redio na televisheni inaruhusu serikali kudhibiti vyombo hivyo.

Aidha nchini humo sheria ya usalama wa taifa inaangalia jinsi habari zinavyotolewa kwa wananchi ambapo kutoa au kuchapisha habari zisizo za kweli ni jambo ambalo limebakia kuwa kosa na mwandishi anaweza kutozwa faini kubwa.

Sheria hii inalenga kuzuia uandishi wa masuala tete na nyeti nchini humo.

Serikali ya Tanzania pia inatumia njia za kifedha kuukandamiza uandishi wa masuala nyeti ya ukosoaji kwa kuzuia matangazo ya biashara katika magazeti hayo yanayochapisha habari za kuikosoa serikali.

Lakini kwa mujibu wa mkurugenzi wa habari Tanzania na msemaji wa serikali Kassim Mpenda hakubaliani na suala hilo anasema kwamba uhuru wa vyombo vya habari unazingatiwa sana nchini Tanzania.

Ripoti iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya habari inasema kwamba hali ya kiuchumi imekuwa mzigo kwa vyombo vya habari binafsi nchini Tanzania hali ambayo inavifanya vyombo hivyo kushindwa kuchapisha na wakati huo huo kuweza kujigharamia.

Licha ya hali hii vyombo vya habari nchini humo vimeweza kupanuka na kumejitokeza sauti zinazokosoa serikali na maoni tofauti juu ya hali ya kisiasa inavyokwenda kutoka kwenye vyombo vya habari vya binafsi hadi vinavyomilikiwa na serikali.

Hata hivyo lakini pamoja na panda shuka nyingi radio zinazomilikiwa na watu binafsi zimeongezeka na pia kuna vituo vingi vya televisheni ambavyo sasa vinapeperusha matangazo yake kote nchini Tanzania.

Radio imebakia kuwa chombo muhimu cha kutoa habari kwa idadi kubwa ya watu nchini humo kama ilivyo katika nchi nyingine nyingi za Afrika.

Pamoja na hayo lakini kuna suala la waandishi habari kupewa vitisho,kunyanyaswa na kupewa mkongo’to.

Mbali na hilo kupata habari pia ni tatizo linalobakia kuwa sugu kwa baadhi ya waandishi habari na kuzuia uwezo wao wa kuripoti.

Mhariri mkuu wa gazeti la’’Mwanahalisi’’ nchini Tanzania Saidi Kubenea ni mmoja kati ya waandishi wanaopokea vitisho kutokana na ripoti zake zinazoibua masuala ya rushwa nchini Tanzania.

Hali ni mbaya zaidi kwa waandishi wa habari katika visiwa vya Zanzibar.

Gazeti la kwanza kabisa la binafsi visiwani humo la Dira limefungiwa hadi hii leo baada kudaiwa na serikali kwamba linakiuka taratibu za kisheria katika kazi yake na linapandikiza mbegu ya chuki kati ya serikali na wananchi wake.