1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mwaka 2007 ya Waandishi wasio na mipaka

1 Februari 2007

Shirika la kimataifa la waandishi habari wasio na mipaka limetoa ripoti yake ya mwaka 2007 kufuatia utafiti wake juu ya uhuru wa vyombo vya habari.

https://p.dw.com/p/CHKu

Ripoti hiyo ya shirika la kimataifa la waandishi habari wasio na mipaka imeashiria washukiwa wa kawaida kama vile China, Korea kaskazini na Cuba kwa kupinga uhuru wa vyombo vya habari.

Na wakati huo ripoti hiyo imekodolea kwa jicho kali visa vinavyohusu ukandamizaji wa demokrasia.

Ripoti hiyo imesema kwamba takriban waandishi habari 81 waliuwawa katika mwaka 2006 na kuufanya mwaka huo kuwa ndio mbaya zaidi katika karne hii.

Irak imetajwa kuwa ndio nchi hatari zaidi kwa wandishi wa habari katika kipindi cha mwaka jana ambako waandishi habari 39 na wadau wengine 26 katika sekta ya uandishi habari waliuwawa.

Shirika hilo la kimataifa la waandishi wasiokuwa na mipaka lenye makao yake mjini Paris Ufaransa limesema kwamba mwaka wa 2006 ulikuwa ni mwaka uliojawa na hatari nyingi dhidi ya wandishi habari kama vile mwaka 1994 wakati kulipotokea mauaji ya halaiki huko nchini Rwanda.

Hali kadhalika katika maeneo kadhaa duniani waandishi wa habari walitupwa ndani ya jela katika mwaka huo wa 2006, takriban waandishi 871 waliwekwa kizuizini huku China ikiongoza kwa kuwaweka korokoroni waandishi habari 32 miongoni mwao akiwemo mwandishi habari anaeripoti kutoka Hong Kong Ching Cheong ambae alihukumiwa kifungo cha miaka mitano.

Cuba inafuata baada ya China kwa uvunjaji wa uhuru wa vyombo vya habari na jumla ya waandishi habari 24 walizuiliwa.

Shirika hilo la kimataifa limemshutumu rais Hu Jintao wa China kwa kuendeleza kampeni inayolenga kuimaliza sekta ya habari na pia mtandao wa internet.

Nchini Ethipoia nako takriban waandhishi habari 21 waliwekwa korokoroni katika mwaka uliopita wa 2006.

Shirika la waandishi wasio na mikapa halikusita kupaaza sauti dhidi ya nchi zinazojiita kuwa ziko mstari wa mbele katika maswala ya kidemokrasia, shirika hilo limesema nchi hizo hazitii bidii au hata zimeachilia mbali nia ya kutetea demokrasia kama zinavyohitajika kufanya.

Wakati wa sakata ya vikatuni vilivyo mkashifu mtume Muhammad S.A.W. jamii ya kimataifa ilishindwa kuwasaidia waandishi habari waliotishiwa maisha yao au hata kukamatwa imesema ripoti hiyo.

Wakati huo huo rais wa Taiwan Chen Shui-bian amemtunukia tuzo ya Asia ya Demokrasia na Utu katibu mkuu wa shirika la waandishi habari wasio na mipaka Robert Menard huku akilisifu shirika hilo sio tu kwa kulinda haki za waandishi wanaokandamizwa na tawala za kidikteta bali pia kutetea demokrasia ya haki na uhuru wa vyombo vya habari duniani kote.