1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mwaka ya Amnesty International

Maja Dreyer23 Mei 2007

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya shirika kubwa zaidi duniani la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, vita dhidi ya ugaidi vinaathiri sana hali ya haki za binadamu duniani. Shirika hilo lina mtandao mkubwa wa wachunguzi duniani kote. Pamoja na kuwasaidia wahanga wa ukiukaji wa haki za binadamu, shirika hilo linajihusisha pia kufahamisha juu ya hali ya haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/CB40
Nembo ya shirika la Amnesty International
Nembo ya shirika la Amnesty International

Hofu ndiyo ina ushawishi mkubwa katika sera za kimataifa. Haya ni kulingana na ripoti ya mwaka wa 2007 ya shirika la Amnesty International ambayo inazungumzia hali ya haki za binadamu duniani katika mwaka wa 2006. Serikali na makundi ya wanamgambo yanawatia watu hofu, na hivyo kuvunja haki za binadamu pamoja na kuigawa dunia. Ripoti hii inasema katika nchi nyingi inapaswa kuhofia mashambulio au vitendo vya uhalifu, lakini ikiwa sera za hofu zinafanikiwa, watu wanaigawa dunia katika makundi tofauti, yaani “sisi” na “wao”, marafiki na maadui, Wakristo na Waislamu.

Barbara Lochbihler ni katibu mkuu wa tawi la Ujerumani la Amnesty International, naye anasisitza: “Tunayaona haya katika maeneo mengi. Wakati huo huo serikali zinajaribu kutumia sera hizo za kuchochea hofu ili kuvunja haki za binadamu na sheria za kidemokrasia.”

Ripoti ya shirika la Amnesty Internation inakumbusha pia kuwa mamia ya watu duniani wanakabiliwa na umaskini na maradhi kama ukimwi,. na bila ya jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za maana. Kuhusu mkutano wa viongizi wa nchi nane zinazostawi kiviwanda duniani G8 mwezi ujao nchini Ujerumani, Bi Lochbihler alitoa mwito kwa viongizi hao kutimiza ahadi zao za kuimarisha taasis zinazoshughulikia haki za binadamu barani Afrika.

Kama mfano alitaja kamati ya haki za binadamu na za makabila pamoja na mahakama ya Kiafrika ambayo bado haijaanza kazi zake.Vile vile, shirika la Amnesty International katika ripoti yake inawataka viongizi wa nchi za G8 wahakikishe kuwa vikwazo vya kupeleka silaha Sudan vinatekelezwa, hasa na China ambayo pia imealikwa kwenye mkutano huo wa kilele wa G8.

China yenyewe imelaumiwa katika ripoti hiyo, pale inaposema kuwa mwaka mmoja kabla ya kufanyika michezo ya Olympics , China bado haikutimiza ahadi za kuboresha haki za haki za binadamu.

Akizungumza ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wakimbizi wa kutoka Afrika wanaoshikwa kwenye mipaka ya nchi za Ulaya, Bi Lochbihler amesema shirika lake la Amnesty International linasikitishwa hasa na “Kwamba mamia ya wakimbizi walirudishwa Marokko kutokana na makubalio yaliyofikiwa baina ya Umoja wa Ulaya na Marokko, na halafu watu hao walipelekwa katika eneo la jangwa na kuachwa huko. Tumegundua kuwa watu wengi walipigwa, na wanawake waliporwa. Ni jambo lisiloweza kukubaliwa kuwa Umoja wa Ulaya unakubali maafikiano bila ya kudhibitisha kwamba haki za msingi za binadamu zitahakikishwa.”

Hapa pia, wanasiasa wanatumia sera za kuchochea hofu, yaani hofu dhidi ya wakimbizi wanaokuja Ulaya kwa wingi. Badala yake, Amnesty International inataka kupambana na vyanzo vya uhamiaji na kuruhusu wakimbizi kuingia Ulaya kwa njia inayosimamiwa vizuri.

Katika mwaka wa 2006, rushwa iliyotapakaa iliendelea kuyaathiri mataifa ya Kiafrika, wakati shida zilipozidishwa na umaskini. Matokeo yake ni hali mbaya ya wasiwasi. Bara hilo sasa linakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kujiingiza China ambayo inajulikana kutozijali haki za binadamu katika sera zake za nje, alisema katibu mkuu wa shirika la Amnesty International, Bi Irene Khan. Shirika hilo linaukosoa Umoja wa Afrika kushindwa kutetea haki za bindamu katika nchi wanachama kama vile Zimbabwe. Pamoja na nchi nyingine zilizotajwa katika ripoti hiyo ya mwaka ni Kenya inayolaumiwa kuwasumbua waandishi wa habari.