1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mwaka ya WHO kuhusu Malaria yaleta matumaini

Zainab Aziz
13 Desemba 2016

Ripoti ya Shirika la afya duniani WHO kuhusu ugonjwa wa Malaria, inaleta matumaini lakini wakati huo huo inatoa tahadhari kwamba ugonjwa huo bado ni tishio kwa jamii hasa katika nchi zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara

https://p.dw.com/p/2UBiK
Symbolbild Tropenkrankheiten Malaria Duengefieber & Co
Picha: Getty Images/Tony Karumba

Kuna habari njema kutokana na ripoti hiyo ya mwaka ya shirika la afya duniani WHO kuhusu Malaria kwamba uwezekano upo wa kuutokomeza kabisa ugonjwa huo kama matokeo yanavyoonyesha katika baadhi ya nchi.  Mnamo mwaka 2015 nchi 10 na baadhi ya maeneo yaliripoti chini ya visa 150 vya ugonjwa wa malaria. Nchi nyingine 9 ziliorodhesha kati ya visa 150 na 1000 kwa ajili hiyo Shirika la Afya duniani WHO linaamini kuwa juhudi za kuutokomeza ugonjwa huo japo katika nchi 10 zinaweza kufua dafu hadi kufikia mwaka 2020.

Perdo Alosno ni mkurugenzi wa WHO anayesimamia mpango wa kupambana na Malaria anasema jambo la muhimu ili kupatikana kwa mafanikio na kuboresha huduma za afya kwa watoto na akina mama wajawazito, hii ni pamoja na kuboresha njia za kubainisha magonjwa na kutoa maelekezo ya tiba katika vituo vya afya vya umma.  Na katika hilo WHO inaweza kujivunia baadhi ya mafanikio.  Dr. Alonso amesema, kuna ongezeko la asilimia 77 katika kipindi cha miaka mitano kwa wanawake wanaopata dozi tatu za kuzuia Malaria wakati wakiwa wajawazito na pia kunaongezeko kubwa katika kueneza vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa kwa jamii ambayo inakabiliwa na hatari ya ugonjwa wa Malaria. 

Malariabekämpfung in Sambia
Operesheni tokomeza Malaria nchini Zambia Picha: picture-alliance/ dpa

Mkakati wa WHO wa kutokomeza Malaria unalenga kupunguza ugonjwa huo kwa asilimia 40 kufikia mwaka 2020.   Hata hivyo nchi nyingi hazina uwezo wa kupambana kikamilifu na Malaria.  Ripoti ya Shirika la Afya duniani WHO inaeleza kuwa nusu ya nchi 91 na maeneo yanayokabiliwa na ugonjwa huo wa Malaria yanakaribia kulifikia lengo la kuungamiza ugonjwa huo. 

Mwandishi: Zainab Aziz
Mhariri:Josephat Charo