1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya njaa ya kila mwaka imetolewa leo

Zainab Aziz
12 Oktoba 2017

Ni kiwango gani cha njaa kilichopo duniani kote kwa nini kuna njaa? Ripoti ya kila mwaka inaonyesha hali ya njaa duniani pamoja na udhaifu wake. Je tatizo kubwa ni ukosefu wa usawa?

https://p.dw.com/p/2lhSf
Infografik Welthungerindex 2017 ENG ***SPERRFRIST BIS 12.10.2017 (10:00 Uhr CEST)***

Ripoti ya kila mwaka kuhusu njaa duniani imechapishwa hivi leo ikionesha kuwa licha ya njaa kupunguwa kwa zaidi ya robo moja tokea mwaka 2000, migogoro ya kisiasa, ukosefu wa usawa wa kijinsia na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi bado ni vichocheo vikubwa kwenye kuendelea kuwapo kwa ukosefu wa chakula miongoni mwa watu wengi duniani.

Si jambo jipya kusikia kuwa umaskini na njaa vikihusishwa pamoja, lakini kuenea kwa janga la njaa katika maeneo tofauti ulimwenguni sio tu kwa sababu ya umasikini, bali pia hutegemea nguvu za kisiasa. Rais wa taasisi ya Welthungerhilfe, Bärbel Dieckmann, amesema katika mahojiano ya DW kwamba usawa haulingani. Mara nyingi wanawake hutendewa tofauti, na hiyo pia hutegema mtu anatoka kwenye kabila gani. Kulingana na Dieckmann anatoa mfano wa nchini India ambako ingawa kuna idadi kubwa ya mabilionea lakini bado takriban watu milioni 200 wanaathiriwa na njaa.

Jitihada zimefanikiwa?

Kwa mara ya kwanza, jitihada za kimataifa za kupambana na njaa zimeonyesha mafanikio ikilinganishwa na alama zinazotolewa duniani (WHI) kwa mwaka wa 2000. Kiwango katika alama hizi za WHI kwa wastani kimepungua kwa asilimia 27, lakini maendeleo au mafanikio hayasambazwi kwa usawa. Kuna nchi 14 zilizoboresha mfumo wake wa chakula kwa asilimia 50.

Infografik Welthungerindex 2010
Makadirio ya kiwango cha njaa katika baadhi ya nchi za Afrika

Katika mwaka huu hali ya njaa duniani kwenye nchi saba inaelezwa kuwa "mbaya sana" na katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, hali hiyo inaelezwa kuwa ni  "mbaya". Mnamo mwaka wa 2000, hali katika nchi nane ilielezewa kuwa ni "mbaya". Hata hivyo, nchi kumi na tatu, ikiwa ni pamoja na Somalia, Sudan Kusini na Syria, hazikujumuishwa katika ripoti ya mwaka huu kwa sababu hakuna taarifa za kutosha kuzihusu. Shirika la WHI hukusanya taarifa juu ya utapiamlo, vifo vya watoto pamoja na matatizo yanayozuia ukuaji wa kasi kwa watoto na taarifa hizi hufanyiwa mukhtasari wake na shirika hilo.

Hitilafu ya mifumo inasababisha njaa

Bärbel Diechmann wa shirika la Welthungerhilfe anasema iwe ni njaa katika kanda au katika nchi hili ni suala la usambazaji na pia ulimwenguni lisingekuwa tatizo kuwalisha binadamu wote leo hii lakini "usambazaji haufanyiki vizuri,"  Naye Hansmann kutoka jopo la wataalamu wa kimataifa, linalohusika na chakula IPES ambalo pia ni jopo la wanasayansi kutoka duniani kote wanaoshughulikia masuala ya lishe na kilimo endelevu. Mtaalamu huyo wa kilimo na maendeleo alishiriki katika ripoti ya Mazingira ya Dunia  yam waka 2008 na alipewa Tuzo ya Maisha Bora, ambayo ni tuzo mbadala ya Nobel kwa ajili ya kazi yake ya mwaka 2013.  Mtalaamu huyo amesema mageuzi katika mlolongo wa vyakula ni muhimu kwa sababu nyingi. Amesema kwanza, tunahitaji kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, pili, ni lazima tuhakikishe kuwa kilimo hakiendelei kuathirika na mabadiliko ya hali ya hewa, na tatu, ni lazima tuhakikishe chakula chenye afya kwa wote.

Kwa miaka mingi, shirika la Welthungerhilfe limejaribu kutekeleza mawazo haya duniani kote katika miradi. Katika mafunzo inayotoa, mbinu za kilimo endelevu zinajumuishwa katika usimamizi wa mashamba.  Ili mpango  mzima uweze kufanya kazi, Bärbel Dieckmann, amesema ni muhimu sana kupatikana elimu ya kisiasa kwa makundi ya watu maskini. Dieckmann anasema katika jamii nyingi kuna nafasi za kushawishi kwa mtu kuweza kuchangia, anasema wawakilishi wa serikali za mitaa watahusishwa katika miradi. Kwa sababu wakati mwingine wawakilishi wa serikali hawafahamu makubaliano ya kimataifa.

Mwandishi: Jeppesen, Helle/Zainab

Mhariri: Mohammed Khelef