1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya SIPRI: Watengenezaji wa silaha wakubwa duniani

10 Desemba 2018

Ripoti ya taasisi ya utafiti wa masuala ya Amani duniani SIPRI imeitaja Marekani kuwa ndiyo inayoongoza katika utengenezaji na uuzaji wa silaha duniani kati ya watengenazaji wakubwa 100 ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/39n7J
Deutschland Waffenproduktion & Waffenexport | Heckler & Koch - Messe Eurosatory in Paris
Picha: picture-alliance/dpa/D. Fischer

Taasisi ya Utafiti wa Amani (SIPRI) imesema ongezeko la utengenezaji na uuzaji wa silaha linajumuisha kuendelea kuimarika miongoni mwa kampuni za kutengeneza silaha ulimwenguni ambapo nchi za Ulaya,Urusi na kwingineko ulimwenguni zimeongeza matumizi kwenye bajeti zake za kijeshi.

Kwa mujibu wa Pieter Wezeman, mtafiti mwandamizi wa masuala ya silaha na matumizi kwenye taasisi ya SIPRI, amesema mauzo ya silaha yamekuwa yanaongezeka kwa silimia 2.5 kwa mwaka.

Taasisi hiyo ya utafiti wa masuala ya amani duniani, SIPRI imesema kampuni za Marekani ndizo zinazoongoza duniani kote katika uuzaji wa silaha za kijeshi. Zaidi ya asilimia 50 ya mauzo hayo yalifanyika mwaka jana ambapo kampuni za Marekani ziliuza silaha za kijeshi zenye thamani ya dola bilioni 44.

Katika ripoti iliyochapishwa leo Jumatatu, SIPRI imesema makampuni 100 makubwa duniani yaliuza silaha za thamani ya jumla ya dola bilioni 398 katika mwaka wa 2017 hilo likiwa ongezeko la mauzo kwa mwaka wa tatu mfululizo. Hiyo inamaanisha uuzaji huo umekuwa kwa asilimia 2.5.

Mpangilio wa kampuni zinazotengeneza na kuuza silaha
Mpangilio wa kampuni zinazotengeneza na kuuza silaha

Marekani inaongoza kwa asilimia 57 wakati ambapo kampuni kubwa za ulinzi za nchini Ujerumani zikiwa katika nafasi ya 25 kati ya kampuni 100 duniani. Urusi, Uturuki na China pia zimeongeza utengenezaji wa silaha.

Kampuni za Ujerumani ni miongoni mwa wazalishaji wa silaha wakubwa duniani kati ya jumla ya kampuni 100 duniani, kampuni hizo ni  Rheinmetall, Thyssenkrupp na Krauss-Maffei Wegmann, ambayo hutengeneza nyambizi, meli, mizinga na magari yenye kinga dhidi ya silaha kwa majeshi ya Ujerumani. Pia huuza bidhaa zake nje ya nchi. Kampuni zote tatu ziliongeza faida zao mnamo mwaka 2017.

Ushindani wa kutengeneza silaha kati ya Marekani na nchi kama vile Urusi na China huongeza kasi ya biashara hiyo.

Kampuni ya Marekani ya Lockheed Martin kwa sasa inatenengeneza kombora lenye gharama kubwa ambalo linaweza kuikwepa mifumo ya kawaida ya rada.

Urusi na China tayari zina makombora ya masafa marefu ya aina hii ambayo huruka kwa kasi sana. Rais wa Marekani Donald Trump amepania kuongoza katika ushindani huu wa kutengeneza silaha.

Katika mwaka ujao, Marekani inatarajia kuwekeza jumla ya dola bilioni 716 katika mpango wa kutengeneza silaha na vifaa vya kijeshi.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPA/p.dw.com/p/39lx3

Mhariri: Yusuf Saumu