1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti yaonyesha uwezekano kuwa Arafat aliuawa kwa sumu

7 Novemba 2013

Wanasayansi wa Uswisi wamesema upo uwezekano kwamba aliyekuwa kiongozi wa wapalestina, Yasser Arafat, aliuawa kwa sumu aina ya polonium, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti iliyoonwa na shirika la habari la Al-Jazeera.

https://p.dw.com/p/1ADQp
Kiongozi wa zamani wa wapalestina, Yasser Arafat ambaye yumkini alilishwa sumu
Kiongozi wa zamani wa wapalestina, Yasser Arafat ambaye yumkini alilishwa sumuPicha: Getty Images

Ripoti hiyo ya wanasayansi kutoka hospitali ya chuo kikuu cha Lousanne nchini Uswisi ndio ya kwanza muhimu kutolewa katika uchunguzi unaofanywa kubainisha kilichomuuwa Yasser Arafat miaka tisa iliyopita.

Mwaka jana wanasayansi hao waligundua dalili za sumu hatari aina ya Polonium-210 katika vifaa vya marehemu Arafat, na baadaye wakayafukuwa mabaki ya mwili wake na kuchukua sampuli za mifupa na za udongo kutoka ndani ya kaburi lake ili vifanyiwe uchunguzi wa kimaabara.

Ushahidi wa kadri

Matokeo ya uchunguzi huo yalichapishwa katika ripoti ya kurasa 108 iliyotolewa jana, ikisema upo ushahidi wa kiwango cha kadri kuunga mkono dhana kwamba Arafat aliuawa kwa sumu.

Mjane wa Arafat, Suha, amekiambia kituo cha televisheni cha al-Jazeera kuwa amehuzunishwa na kushtushwa na yaliyomo katika ripoti hiyo, na kuapa kuchukua hatua.

Suha Arafat na mmewe alipokuwa bado hai
Suha Arafat na mmewe alipokuwa bado haiPicha: picture-alliance/dpa

''Sitasita, mimi na binti yangu tutakwenda katika mahakama zote za dunia, ili mtu aliyefanya uhalifu huu aadhibiwe.'' Alisema Bi Suha Arafat.

Mjane huyo ameendelea kusema kuwa atataka uchunguzi ufanywe katika makao makuu ya serikali ya ndani ya wapalestina yajulikanayo kama Muqata, na kusisitiza kwamba yeye na binti yake Zahwa watachukuwa hatua zozote zinazowezekana.

Kamati ya wapalestina inayochunguza kifo cha aliyekuwa kiongozi wao imepewa nakala ya ripoti hiyo ya wanasayansi, lakini imekataa kutoa tamko lolote. Mkuu wa kamati hiyo, Tawfiki Tirawi, amesema watatoa maelezo kwa vyombo vya habari katika muda wa siku mbili, na watatangaza vile vile hatua ambazo wanaweza kuzichukua.

Ripoti yaondoa utata

Yasser Arafat alifariki Novemba mwaka 2004, mwezi mmoja baada ya kupatwa na maradhi makali katika makao yake mjini Ramallah. Madaktari Wafaransa waliomtibu walisema alikufa kutokana na matatizo makubwa ya moyo, na maambukizi fulani katika mfumo wake wa damu.

Mtaalamu wa masuala ya ushahidi wa kimahakama, Profesa David Barkley, kutoka Uingereza ameiambia al-Jazeera kwamba hana shaka yoyote kuhusu kilichomuuwa Arafat.

Bendera ya Palestina, nchi ambayo haijapata hadhi ya utaifa
Bendera ya Palestina, nchi ambayo haijapata hadhi ya utaifaPicha: picture-alliance/dpa

''Kama ningekuwa kwenye jopo la majaji, nisingeona utata wowote katika kisa hiki. Kwa maoni yangu hakuna shaka lolote kwamba ni sumu ya polonium iliyoyaangamiza maisha ya Arafat.'' Profesa Barkley amesema.

Mtaalamu huyo kutoka Uingereza amesema ripoti iliyotolewa ni ushahidi tosha juu ya kilichosababisha ugonjwa wa Arafat, ambacho amesema kilitolewa kwake kwa nia mbaya.

Israel yasutwa kidole

Mjumbe wa kamati kuu ya chama cha ukombozi wa Palestina, PLO, katika maeneo ya wapalestina, Wasel Abu Youssef, amesema Yasser Arafat aliuawa kupitia ugaidi unaodhaminiwa na taifa la Israel.

Israel lakini imejitenga mbali na shutuma hizo. Aliyewahi kuwa msemaji wa serikali yake, Raanan Gissin, amesema ilikuwa sera ya serikali ya Israel kutomgusa Arafat, na kuongeza kwamba nchi hiyo haikuhusika kwa vyovyote na kifo cha kiongozi huyo. Gissin amesema ripoti ya wanasayansi ni mchezo wa kuigiza, katika kile alichosema ni njama ya mjane wa Arafat kuwawekea vipingamizi waliorithi madaraka yake.

Ripoti ya wanasayansi wa Uswisi imetumia lugha yenye tahadhari kubwa, ikisema zilikuwepo kasoro kadhaa za kiuchunguzi kama vile muda mrefu uliopita tangu kifo cha Arafat hadi pale uchunguzi ulipoanza na ubora wa sampuli zilizopatikana.

Mwandishi. Daniel Gakuba/RTRE/APE

Mhariri: Josephat Charo