1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Roberto Avezedo ndiye kiongozi mpya wa WTO

9 Mei 2013

Umoja wa Ulaya, Marekani na China ni miongoni mwa nchi ambazo zimesema zitamuunga mkono mkuu mpya wa Shirika la Biashara Duniani – WTO, Mbrazil Roberto Avezedo.

https://p.dw.com/p/18UoG
File picture shows Roberto Azevedo, Brazil's permanent representative to the World Trade Organization (WTO), during an interview with Reuters in London in this March 14, 2013 file photo. Azevedo, a Brazilian trade diplomat, will be the next head of the World Trade Organization, a diplomatic source said on May 7, 2013 after the results of the contest to succeed France's Pascal Lamy were given in a confidential meeting. REUTERS/Luke MacGregor/Files (BRITAIN - Tags: POLITICS BUSINESS TPX IMAGES OF THE DAY)
Neuer WTO-Chef Roberto AzevedoPicha: Reuters

Azevedo alimshinda mgombea mwenzake Herminio Blanco wa Mexico ambaye alikuwa akipigiwa upatu na Marekani pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya katika duru ya mwisho ya kinyan'ganyiro hicho kuchukuwa nafasi ya Pascal Lamy ambaye anan'gatuka hapo mwezi wa Augosti. Roberto Avezedo mwenye umri wa miaka 55 na ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Brazil katika Shirika la Biashara Duniani – WTO, alipata uungwaji mkono mkubwa kutoka nchi zinazoinukia kiuchumi duniani.

Kaimu mwakilishi wa Marekani kuhusu biashara Demetrios Marantis amesema Marekani imefurahishwa na uamuzi wa pamoja wa kumteuwa Roberto Azevedo kama Mkurugenzi mkuu wa WTO, na inatazamia kufanya kazi naye na wanachama wengine katika kulifanya shirika hilo kuwa imara, na lenye mafanikio katika siku zijazo.

Naye Kamisha wa Biashara katika Umoja wa Ulaya Karel De Gucht amesema anaamini Azavedo atasaidia kuyafufua mazungumzo ya kibiashara yaliyokwama ya Doha, wakati wa mkutano wa mawaziri wa WTO mjini Bali mwezi Desemba. Mazungumzo ya Doha ambayo yalianzishwa katika mkutano wa kilele nchini Qatar mwaka wa 2001, yanalenga kufikia muafaka kuhusu kufungua biashara na kuondoa vizingiti vya kibiashara kama vile ruzuku, kodi nyingi kupindukia, na kanuni za kushirikisha biashara ya kimataifa kuzisaidia nchi maskini. Azevedo amezitaka nchi zinazolumbana kuitathmini misimamo yao kwa sababu shirika la WTO lina umuhimu katika maisha ya kila mwananchi kote ulimwenguni, iwe wanalifahamu hilo au la. Ujumbe mwingine umetolewa na Canada ambayo imemtaka kiongozi huyo mpya kukabiliana na kitisho kinachosababishwa na ulinzi wa masoko katika juhudi za kuufufa uchumi wa ulimwengu.

Mgombea Herminio Blanco alipigiwa upatu na Marekani na Nchi za Umoja wa Ulaya
Mgombea Herminio Blanco alipigiwa upatu na Marekani na Nchi za Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/dpa

China imeukaribisha uteuzi huo ikisema umedhihirisha mshikimanano mkubwa wa nchi nchi zinazoinukia kiuchumi. Shirika la Habari la China limesema uteuzi wa Azevedo ni kitu cha kujivunia kwa sababu ndio mara ya kwanza kwa mgombea kutoka kundi la nchi zinazoinukia kiviwanda BRICS- yaani Brazil, China, India, Urusi na Afrika Kusini, amepewa wadhifa huo.

Akizungumzia uteuzi wake, Azevedo amewashukuru wagombea wenzake wanane walioshiriki katika kinyang'anyiro hicho, akisema kuwa kiwango chao cha ujuzi na utaalamu kilimanaanisha kuwa pangekuwa na Mkurugenzi Mkuu mpya mwenye ubora wa hali ya juu, bila kuzingatia yule angechaguliwa.

Katika taarifa, rais wa Brazil, Dilma Roussef amesema chaguo la Azevedo ni ushindi kwa shirika zima la WTO. WTO humchagua kiongozi wake kwa misingi ya maelewano na wala siyo kupitia uchaguzi. Shirika la Biashara Duniani limesema Azevedo ataidhinishwa rasmi na nchi wanachama mnamo Mei 14 na kisha kuchukua rasmi wadhfa huo mnamo Septemba mosi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri:Yusuf Saumu